Wanafunzi waliofanya vizuri Umisseta, Umitashumta kuitwa timu ya Taifa

Mariam John 1105Hrs   Julai 01, 2024 Habari
  • Ni kwa ajili ya kuendeleza vipaji na kutanua wigo wa ajira.
  • Mwanza yaendelea kutamba Umitashumta, yaibuka mshindi wa jumla na vikombe 21.


Mwanza. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amemuagiza Mkurugenzi wa Michezo nchini, Ally Mayay kuwajumuisha kwenye timu za taifa wanafunzi watatu waliofanya vizuri kwenye mashindano ya Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) na yale ya sekondari (Umisseta) kutoka Mwanza.

Ndumbaro aliyekuwa akizungumza leo Julai 1, 2024 jijini Mwanza wakati akipokea makombe 21 yaliyobebwa na timu za mkoa huo kwenye mashindano ya Umitashumta na Umisseta yaliyofanyika mkoani Tabora  amesema wanafunzi hao wanatakiwa kuungana na wachezaji wazoefu ili kupata uzoefu wa mashindano makubwa.

Wanafunzi wanaotarajiwa kuunganishwa kwenye timu ya taifa ni pamoja na Magreth Manawa mfungaji bora wa mpira wa pete (Netiboli), Neema Mkula na mchezaji bora wa Pete, Agness Charles.

“Wizara imeshatoa maelekezo kwa vyama vyote vya michezo nchini wanapoita timu za taifa lazima wajumuishe angalau wachezaji wawili, mmoja kutoka Umisseta na mwingine wa Umitashumta ili kuendeleza vipaji hivyo na kuingia kwenye timu za taifa,” amesema Ndumbaro.

Aidha, Ndumbaro amebainisha kuwa wachezaji wote waliochaguliwa na maskauti wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) nao watajumuishwa kwenye timu za taifa ili kuendeleza vipaji vya wanafunzi hao jambo litalosaidia kutanua wigo wa ajira.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amesema uongozi wa mkoa wake utahakikisha mkoa huo unakuwa namba moja kwenye kila jambo zuri wanaloshiriki na kuwaunga mkono wanamichezo wa Mwanza, huku wakijipanga kuanzisha shindano la kusaka vipaji (Mwanza Star Search).

Mtanda ameongeza kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa kuunga juhudi za kukuza sekta ya sanaa zinazofanywa na Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Basuta).

Mkoa wa Mwanza umeibuka mshindi wa jumla wa michezo katika mashindano ya Umisseta na Umitashumta kwa kutwaa vikombe 12 vya Umitashumta na tisa vya Umisseta.

Kwa mujibu wa Afisa Michezo wa Mkoa wa Mwanza James William, mkoa huo umeendelea kushika nafasi ya kwanza Umitashumta kwa miaka mitatu mfululizo na nafasi ya kwanza Umisseta kwa mara ya kwanza.

Ambapo timu za mpira wa pete, riadha kwa  wasichana, wavu kwa wavulana, soka kwa wasichana na kikapu wavulana na wasichana zitashiriki mashindano ya Afrika Mashariki (Feasssa) Agosti mwaka huu nchini Uganda.

Magreth Manawa aliyekuwa mchezaji bora wa kikapu kwa wasichana ambaye amejumuishwa timu ya taifa amesema hatua hiyo ni faraja kwake na imempa moyo kuona Serikali na wadau wanaunga mkono vipaji vichanga.

“Ndoto yangu ni kupiga hatua na kucheza mchezo wa kikapu nchini Marekani kupitia ufadhili wa masomo ili nipate kipato na ajira,  nawaomba wazazi watoe ruhusa na sapoti kwa watoto wao wenye vipaji,” amesema Manawa.

Related Post