Ahueni: Bei za mafuta zashuka kiduchu Tanzania

Esau Ng'umbi 0433Hrs   Julai 03, 2024 Biashara
  • Petroli yashuka kwa Sh52 kwa lita kwa bei ya rejareja, dizeli yapanda kwa Sh3 na mafuta ya taa yasalia bei ile ile ya mwezi Juni.
  • Ahueni hiyo inatokakana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kwa wastani (weighted average).

Dar es Salaam. Maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini yameendelea kupungua kidogo kwa mwezi Julai mara baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kushuka kwa mwezi wa pili mfululizo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Julai 3, 2024 inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh51.

Hata hivyo, bei ya reja reja ya dizeli iliyopita katika bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kidogo kwa Sh3 kwa lita huku ya mafuta ya taa ikisalia ile ile iliyokuwepo mwezi uliopita.

Katika bei hizo mpya, wakazi wa Dar es Salaam watanunua petroli kwa reja reja kwa Sh3,210 kwa lita kutoka Sh3,261 iliyotumika mwezi Januari huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh3,115 kwa lita kutoka 3,112 iliyorekodiwa mwezi uliopita.




Mafuta ya taa sasa Dar es Salaam yanaendelea kuuuzwa Sh3,261 kwa lita kama ilivyokuwa mwezi Juni 2024.

Kwa upande wa mafuta yanayoingizwa kupitia Bandari ya Tanga  lita moja ya petroli itanunuliwa kwa Sh3,210 kutoka Sh3,263 ya mwezi uliopita.

Dizeli inayotumika zaidi kwenye mitambo na vyombo vya moto, sasa itanunuliwa kwa Sh3,124 kwa lita kutoka Sh3,121 wakati mafuta ya taa kwa Sh3,307 iliyokuwepo mwezi Juni.

Watu wanaotumia mafuta yaliyopitia Bandari ya Mtwara watanunua petroli kwa Sh3,212 kwa lita kutoka Sh3,267 mwezi Juni 2024, dizeli Sh3,124 kutoka Sh3,122  na mafuta ya taa yanasalia bei ile ile ya Sh 3,333 kwa lita.

Kwa mujibu wa Ewura, kupungua kwa bei za mafuta kwa mwezi Julai 2024 kunatokana na kushuka kwa bei za mafuta yaliyochakatwa  (FOB) katika soko la dunia kwa wastani (weighted average) kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Hata hivyo, ahueni hiyo katika bei ya mafuta nchini haipunguzi maumivu kwa watumaiji wa nishati hiyo kwa kiasi kikubwa hasa wa kipato kidogo kutokana na kushuka kwa kiwango kidogo. 

Related Post