Sio Kweli: Gen Z wachoma moto ndege ya Rais wa kenya

Daniel Mwingira 0942Hrs   Julai 03, 2024 NuktaFakti
  • Ndege iliyochomwa ilikuwa ikitumika kama mgahawa katika bustani ya Uhuru.
  • Eneo ilipo ndege hiyo ni katikati ya mji na si sehemu ya ndege kutua.


Dar es Salaam. Kwa wiki ya pili sasa nchi ya Kenya imekuwa haina utulivu kutokana na maandamano ya kupinga muswada mpya wa Sheria ya Fedha nchini humo yanayoongozwa na vijana wa kizazi kipya maarufu kama ‘Gen Z’.

Hata hivyo, watu wenye nia ovu wametumia fursa ya maandamano hayo kuandaa taarifa nyingi za uzushi ambazo zimekuwa zikisambazwa katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, X (zamani Twitter) pamoja na TikTok.

Miongoni mwa taarifa hizo ni ile inayoendelea kusambaa hivi sasa kwenye mitandao ya X na TikTok, ikidai kuwa vijana wa kizazi kipya wanaoongoza maandamano maarufu wa Gen Z wamechoma moto ndege ya rais wa Kenya aina ya Jet.

Madai ya Kuchomwa kwa Ndege

Video hiyo imekuwa ikisambaa ikiwa na maandishi ya lugha ya Kiingereza yanayosomeka “KENYA'S JET SET ABLAZE BY RAMPAGING YOUTH. Angry Kenyan youth have burnt down a presidential private jet being used by their president. This is the shape of things unfolding in Africa, Amen."

Kwa tafsiri ya kimantiki, ujumbe huu unamaanisha: "JETI YA KENYA YATEKETEZWA KWA MOTO KUTOKANA NA GHADHABU YA VIJANA. Vijana wenye hasira nchini Kenya wamechoma moto ndege ya binafsi ya Rais ambayo iliyokuwa ikitumiwa na Rais wao, Haya ndiyo yanayoendelea kutokea barani Afrika. Amina."

Katika video hiyo, vijana wanaonekana wakisukuma ndege na kisha kuichoma moto. Pia sehemu ya video hiyo inadai kuwa vijana wa Gen Z wanachoma kila kitu wanachokiona cha Serikali kutokana na wabunge wote wa nchi hiyo kupiga kura ya kuunga mkono muswada huo.

Ukweli Huu Hapa!

Ufuatiliaji na uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa hakuna ndege yoyote ya Rais wa Kenya aina ya Jet iliyochomwa moto.

Kwa msaada wa Google Reverse Image, imebainika kuwa picha na video hizo zinaonyesha eneo la Uhuru Park, katikati ya mji wa Nairobi, hivyo sio eneo ambalo kuna kiwanja cha ndege ambapo ndege inaweza kutua bali ni eneo la mapumziko.

Pia, ndege hiyo ambayo ipo katika eneo la Uhuru Park ni ndege chakavu aina ya Boeing 737 ambayo imegeuzwa kuwa mgahawa. 

Picha za Google za Agosti 30, 2022, zinaonyesha ndege hiyo ikiwa katika eneo hilo.

Historia ya Uhuru Park

Bustani ya Uhuru Park ilitangazwa rasmi na kufunguliwa kwa umma na Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, tarehe 23 Mei 1969 kama ishara ya uhuru wa nchi. 

Aidha, ni makazi ya mnara wa wapigania uhuru wa Mau-Mau unaoheshimu waathiriwa wa mateso wakati wa enzi ya ukoloni.

Tofauti ya Ndege

Ndege ya Rais wa Kenya ni tofauti kabisa na ile inayoonekana kwenye video. Ndege ya Rais wa Kenya ina rangi nyeupe yenye maandishi ya "Republic of Kenya" (Jamhuri ya Kenya). 

Hii inaweza kuthibitishwa kwa video mbalimbali za ndegehiyo, ikiwemo zile za mwaka 2019 na 2023.

Habari za zamani

Pia, kuna habari za picha ya ndege hiyo hiyo iliyosambaa mwaka 2012 ikisema kuwa ndege ya rais wa Kenya imetua kwa dharura. 

Habari hiyo ilifanyiwa uthibitisho na PesaCheck na kubainika kuwa sio tukio la kweli.

Kwa hivyo, madai ya kuchomwa kwa ndege ya rais wa Kenya ni ya uongo na yamebainishwa kama uzushi.

Gen Z ni kina nani?

Gen Z inasimama badala ya maneno Generation Z au Zoomer. Ambapo inarejea kuanzia kizazi kilichofuata baada ya millennia, na kinajumuisha watu waliyozaliwa kati ya mwaka 1995 na 2010.

Related Post