Makamba: Safari za Rais Samia zina uhusiano na ustawi wa wananchi

Lucy Samson 0802Hrs   Juni 06, 2024 Habari
  • Asema kuna uhusiano mkubwa kati ya safari hizo na maendeleo ya nchi.
  • Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu abainisha ilichovuna Tanzania kutokana na ziara ya Rais nchini Korea


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba amesema ziara za Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi zina uhusiano wa moja kwa moja na ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Makamba aliyekuwa akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam ulioandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Juni 6, 2024 amesema kuwa ziara hizo zinalenga kupanua ushirikiano wa kimataifa katika sekta mbalimbali hususani ya kiuchumi.

“Kuna dhana kwamba safari za nje hazina uhusiano na maendeleo, zina uhusiano mkubwa sana na hazikwepeki na ninyi ni mashahidi tulijaribu kufunga milango na matokeo tunayajua yaliyotokea kwenye uwekezaji na biashara,” amesema Makamba.

Makamba amebainisha kuwa mfano ziara ya Rais Samia iliyoleta matunda ni ile ya nchini India ambapo kupitia mazungumzo kati ya marais wa nchi hizo mbili, mauzo ya zao la mbaazi kutoka Tanzania yaliongezeka kutoka tani 50,000 mpaka tani 250,000.


Kauli ya Makamba inakuja wakati ambapo kumekuwepo na ukosoaji kwa baadhi ya wananchi na viongozi wa vyama pinzani juu safari za Rais Samia nje ya nchi kama zina manufaa kwa wananchi wake.

Mathalani, wadau wa siasa wamekuwa wakielekeza malalamiko yao kwenye gharama kubwa zinazotumika kugharamia safari pamoja na ujumbe unaoambatana na Rais katika ziara hizo.

Uchambuzi wa ziara za Rais Samia uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa kwa mwaka 2024 pekee kiongozi huyo alisafiri katika mataifa 10 ndani na nje ya bara la Afrika.

Miongoni mwa mataifa aliyotatembelea kiongozi huyo nje ya bara la Afrika ni pamoja na Jamhuri ya Korea, Ufaransa, Uturuki, Namibia, Norway, Vatican na Indonesia.

Barani Afrika Rais Samia amezitembelea nchi za Namibia, kenya, Ethiopia na Nigeria.


Soma zaidi:Serikali kushirikisha wadau, wasanii, viongozi wa dini kupambana na uchafuzi wa mazingira


Ilichovuna Tanzania Jamhuri ya Korea

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zuhura Yunus, ziara ya Rais Samia nchini Korea imekuwa na mafanikio mengi ikiwemo kusaini mkataba wa ushirikiano kwa miaka mitano na Jamhuri ya Korea ambao utaiwezesha Tanzania kupata mkopo wa Sh6.5 trillioni kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Mkataba mwingine uliosainiwa ni wa Sh427.8 bilioni za mkopo kwa ajili kuimarisha huduma ya afya na teknolojia ya kisasa katika matibabu pamoja na ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Binguni iliyopo visiwani Zanzibar.

“Mbali na ziara yake alikutana na watendaji wakuu wa makampuni makubwa yanayotarajiwa kuwekeza…kuna kampuni ya KoGas inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi, Dongwon Fisheries masuala ya uchumi wa buluu na kampuni ya Posco inayojihusisha na utengenezaji wa chuma,” amesema Yunus. 

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji amesema kuwa ziara hiyo itafungua fursa za uwekezaji katika maeneo ya madini ya kimkakati, uchumi wa bluu na kilimo ambayo yatawezesha Tanzania kulisha soko la kimataifa na hatimaye kukuza uchumi.

“Tuna uhakika ndani ya miaka mitano mpaka 10 tutakuwa tumeongeza zaidi ya mara mbili ya ambacho tumekifanya kwa miaka 61 iliyopita…wakija hizi kampuni( za uwekezaji) tuwe tayari kujifunza na kufanya kazi kama wao wanavyofanya kazi,” amesema Kijaji.

Related Post