Tanzania yabakiza riba ya benki kuu asilimia 6

Nuzulack Dausen 0256Hrs   Julai 04, 2024 Biashara
  • Riba hiyo ya benki kuu itatumika katika kipindi cha robo ya tatu ya Julai hadi Septemba 2024.
  • Uamuzi huo umetokana na mtazamo chanya wa uchumi wa dunia.
  • Mfumuko wa bei unatarajia kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu mpaka nne katika kipindi cha pili cha mwaka 2024.

Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu imebakiza riba ya benki kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 6 katika robo ya tatu ya mwaka 2024 kutokana na matarajio chanya ya ukuaji wa uchumi wa dunia, kushuka kwa mfumuko wa bei katika mataifa mbalimbali na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani.

Kiwango hicho kilichotangazwa leo Julai 4, 2024 na Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Yamungu Kayandabila ni sawa na kilichokuwa kinatumika katika robo iliyoishia Juni 2024.

CBR ni riba kiongozi ambayo hutumiwa na BoT katika kufanya biashara na benki za biashara nchini. 

Riba hiyo ilianza kutumika kuanzia Januari 2024 baada ya kuanza utekelezaji wa sera mpya ya fedha inayotumia CBR kudhibiti mfumuko wa bei badala ya sera ya ujazi wa fedha.

Dk. Kayandabila amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa kiwango hicho cha riba kitaendelea kutumika kwa kipindi kingine cha Julai hadi Septemba 2024.

Kiwango cha kwanza cha CBR kutangazwa mwaka huu kilikuwa asilimia 5.5 kwa robo iliyoishia Machi na kisha kupandishwa hadi asilimia 6 katika robo iliyoishia Juni.

“Tathmini ya kamati kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha January hadi Juni 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5,” amesema Dk Kayandabila.

Uchumi kukua kwa kasi

Amesema kamati inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi, sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya Shilingi kutokana na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni zinatokanazo na utalii na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula.

Kamati hiyo inayoongozwa na Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba iliridhishwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi.

“Hali hiyo ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, kufuatia hali nzuri ya hewa kwa ajili ya shughuli za kilimo, upatikanaji wa uhakika wa umeme, uboreshaji wa miundombinu hususani reli, barabara na bandari pamoja na sera na program za maboresho.

Takwimu za Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji zinaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania uliendelea kuimarika baada ya kufikia ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 ukichochewa zaidi na ukuaji wa shughuli za biashara na uwekezaji wa sekta binafsi na maboresha ya mazingira ya biashara, uchumi huo unatarajia kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2024.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa miaka mitatu tangu aingie madarakani imekuwa ikipambana kuurejesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwenye viwango vya juu kabla ya athari za Uviko-19 vya asilimia 6 hadi 7.

Hata hivyo, uchumi wa Tanzania umekuwa ukikabiliwa na misukosuko ikiwemo athari za kiuchumi zinazotokana na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine na kushuka kwa thamani ya Shilingi ambako kumechangia pia mfumuko wa bei.

 Mfumuko wa bei watarajiwa kubaki ndani ya wigo

Mfumuko wa bei nchini ulikuwa kati ya asilimia 3 hadi 3.1 ndani ya miezi mitano ya awali ya mwaka 2024 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango ambacho kipo chini ya wigo wa Serikali wa asilimia 5.

Dk. Kayandabila amewaambia wanahabari kuwa kamati hiyo ya fedha sasa inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3-4 katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na kuendelea, ikichagizwa na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, upatikanaji wa chakula cha kutosha, upatikanaji wa uhakika wa umeme na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.

Related Post