Rais Samia atengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa Simiyu, Mkuu wa Wilaya Nanyumbu.

Esau Ng'umbi 0343Hrs   Juni 11, 2024 Habari
  • Amteua Kenan Kihongosi kuwa Mkuu wa Mkoa Simiyu.
  • Uapisho wa viongozi wateule kufanyika baadae.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya panga pangua ya viongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, awamu hii akitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda na Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Dk. Stephen Isaac Mwakajumulo.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu leo Juni 11, 2024 imebainisha kuwa Rais Samia amemteua Kenan Laban Kihongosi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akichukua nafasi ya Dk. Yahaya Ismail Nawanda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo Kihongosi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe ambapo alihamishiwa kushika nafasi iliyoachwa wazi na Fakii Raphael Lulandala aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Hata hivyo, taarifa ya utenguzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu inakuja wakati ambao kumekuwepo na mijadala kumhusu kiongozi huyo kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususan katika mitandao ya kijamii.


Utenguzi huo unakuja ikiwa imepita siku nne tu tangu Rais Samia alipofanya mabadiliko ya viongozi kwenye nafasi mbalimbali za wizara, pamoja na Tamisemi kwa kile kilichodaiwa kuboresha utendaji kazi serikalini.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Rais Samia amemteua Elias Daniel Mwandobo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Momba ambapo kabla ya uteuzi huo Mwandobo alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Christopher Magala, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu akichukua nafasi ya Dk. Stephen Isaac Mwakajumilo ambaye uteuzi wake umetenguliwa na George Hillary Herbert ambaye ameteuliwa kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

“Uapisho wa Mkuu wa Mkoa na Msajili wa Mahakama ya Rufani utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye,” imebainisha taarifa hiyo.

U

Related Post