Rais Samia afanya uteuzi, uhamisho wa viongozi

Esau Ng'umbi 1156Hrs   Juni 06, 2024 Habari
  • Amteua Zuhura Yunus kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
  • Stanslaus Nyongo arejea nafasi ya unaibu waziri, akipangiwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji,


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya viongozi wa nafasi mbalimbali Serikalini kwa kuhamisha na kuteua viongozi wapya akiwemo Mbunge wa Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji.

Nyongo anarejea kwenye Baraza la Mawaziri baada ya kukaa pembeni kwa takriban miaka minne tangu alipoondolewa kuwa Naibu Waziri wa Madini mwaka 2020 nafasi aliyohudumu kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Moses Kusiluka na kuchapishwa na kurasa za Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Juni 6, 2024, Rais Samia amefanya uteuzi huo ili kuboresha utendaji kazi.

“Bi. Felister Peter Mdemu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia masuala ya Jinsia na Wanawake. Kabla ya uteuzi, Bi. Mdemu alikuwa Msaidizi wa Rais, Maendeleo ya Jamii.

Aidha, Bw. Amon Anastaz Mpanju atakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Ikulu.

Taarifa hiyo iliyochapishwa majira ya saa moja usiku imebainisha kuwa Zuhura Yunus Abdallah ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambapo kabla ya uteuzi huo Zuhura alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.



Wengine walioteuliwa ni pamoja na Petro Magoti Itozya aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe huku aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Fatma Almas Nyangasa akihamishwa kutoka wilaya ya Kisarawe na kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa.

Wakati huo huo, Hamis Athumani Mkanachi amehamishwa kutoka Wilaya ya Kondoa kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ambapo taarifa ya ikulu imebainisha kuwa aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Elibariki Bajuta atapangiwa kazi nyingine.

“Bw. Reuben Michael Chongolo amehamishwa kutoka Wilaya ya Songwe kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi na Bw. Frank Mastara Sichwale amehamishwa kutoka Wilaya ya Mufindi kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe,” imebainisha taarifa ya Ikulu.

Pangapangua wakurugenzi watendaji wa halmashauri

Rais Samia amefanya pia mabadiliko kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini ambapo Mussa Abdul Kitungi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia huku Kalekwa Kasanga akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambapo kabla ya uteuzi, Kasanga alikuwa Afisa Sheria Mwandamizi, Tume ya Kurekebisha Sheria.

Wakurugenzi wengine walioteuliwa ni Shaaban Abdulrahman Mpendu alyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Sigilinda Modest Mdemu aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Milton Mailos Lupa aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.

“Bi. Upendo Erick Mangali amehamishwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Babati kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Bw. Kisena Magena Mabuba amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma. 

…Bw. Mabuba anachukua nafasi ya Bi. Mwantum Mgonja ambaye uteuzi wake umetenguliwa; na Bi. Teresia Aloyce Irafay amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang,” inafafanua taarifa hiyo.

Uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu majaji walioteuliwa na Rais Samia ameteua majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Nehemia Ernest Mandia, Projestus Rweyongeza Kahyoza na Mariam Mchomba Omary.

Hata hivyo taarifa ya Kusiluka imebainisha kuwa uapisho wa naibu waziri, naibu makatibu wakuu na majaji wa mahakama kuu utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye.

Related Post