Nyusi: Tumieni maonesho ya kibiashara kukuza mahusiano ya kimataifa

Fatuma Hussein 0939Hrs   Julai 03, 2024 Habari
  • Asema maonesho ya biashara ndio jukwaa linalowaleta wafanyabiashara, wajasiriamali,na kampuni kutoka nchi mbalimbali pamoja.
  • Rais Samia asisitiza ushirikiano wa kitaifa, kimataifa na kikanda ili kujenga uchumi jumuishi na shindani.


Dar es salaam. Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amewataka wafanyabiashara wa Tanzania na wa nchini kwake kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea nchini Tanzania kama chombo cha kukuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia.

Rais Nyusi aliyekuwa akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonesho ya sabasaba leo Juni 3, 2024 Temeke Dar es Salaam, amesema kuwa maonesho ya biashara ndio jukwaa linalowaleta wafanyabiashara, wajasiriamali,na kampuni kutoka nchi mbalimbali pamoja.

“Matarajio yetu kuhusu maonesho haya ni kwamba yatatumika kama chombo cha kukuza  fursa zetu za ushirikano na ubadilishanaji na uwekezaji katika maeneo yetu ya biashara na pia kuanzisha ubia wenye manufaa kwa wote kati ya nchi zetu zote mbili kati ya Msumbiji na Tanzania ,” amesema Nyusi.

Rais Nyusi ameongeza kuwa licha ya kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye athari chanya kwenye uchumi wa mataifa hayo unachukua muda mrefu kukamilika ni muhimu kuendelea kushirikiana ili kutanua uwanda wa fursa za uwekezaji na kufanya biashara za pamoja.

“Jumla ya biashara za nje za nchi zetu mbili katika uagizaji na mauzo ya nje ilifikia karibu Dola milioni 250 tu za nje, mtiririko wa uwekezaji kutoka Tanzania na Msumbiji ilikuwa Dola za Marekani bilioni1.1 kati ya mwaka 2013 na 2023,” amebainisha Nyusi.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaambia wafanyabiashara kuwa Serikali yake iko tayari kusikiliza kero na changamoto zote za wafanya biashara ili kuweka mazingira bora kwa wawekezaji kama kaulimbiu ya maonesho hayo ya 48  inayosema Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni wake Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)  leo Julai 03, 2024. Picha l Ikulu

Rais Samia ameongeza kuwa kauli mbiu hiyo ni nyenzo katika kuchochea sekta mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na ili kujenga uchumi jumuishi na shindani katika nyanja mbalimbali kama viwanda, biashara na uwekezaji ni muhimu kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wa kitaifa, kimataifa na kikanda.

 “Mwaka 2023 kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC ) kimesajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.68 (Tsh15.07 trilioni) hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania, wanaona fursa wanashiriki maonesho … 

Mauzo ya nje ya bidhaa zetu yalipanda kutoka trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi kufikia Shilingi trilion 17.38 sawa na Dola za Marekani bilioni 6.56 mwaka jana  2023..,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia jumla ya kampuni 3,486 za kitaifa na kimataifa zimeshiriki maonesho hayo ya 48 yalioanza Juni 28, 2024 na kutarajiwa kufika tamati Julai 13, 2024.

Maonesho ya 48 Sabasaba yamefunguliwa leo rasmi na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi aliye ziarani nchini Tanzania kwa mualiko wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Related Post