Bajeti ya Serikali Tanzania yapaa hadi Sh49.35 trilioni

Mwandishi Wetu 1105Hrs   Juni 13, 2024 Habari
  • Asilimia 70 ya bajeti hiyo inatarajiwa kutumika kugharamia matumizi ya kawaida ya Serikali.
  • Serikali yatarajia kukopa zaidi ya Sh9.61 trilioni kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi kulipa deni la Serikali na miradi ya maendeleo.

Dar es Salaam. Bajeti kuu ya Serikali ya Tanzania imeongezeka kwa Sh4.96 trilioni ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia Sh49.35 trilioni mwaka wa fedha wa 2024/25 huku theluthi mbili zikitarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Kiwango hicho cha bajeti kimeongezeka kwa asilimia 11.2 kutoka Sh44.39 trilioni zilizopitishwa na Bunge kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2023/24.

Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba amesema bungeni leo Juni 13, 2024 kuwa ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani.

“Ongezeko hilo pia litagharamia ajira mpya ulipaji wa hati za madai, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja,” amesema Dk Nchemba. 

Katika bajeti hiyo inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia Julai mosi mwaka huu, Serikali inatarajia mapato ya ndani kuwa Sh34.61 trilioni ikiwa ni sawa na asilimia 70.1 ya bajeti yote au sawa asilimia 15.7 ya pato la Taifa. 

Dk Nchemba amewaambia wabunge wakati akisoma bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2024/25 kuwa kati ya mapato hayo, yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa Sh29.41 trilioni, mapato yasiyo ya kodi yatakayokusanywa na wizara, taasisi na idara zinazojitegemea ni Sh3.84 trilioni.


Soma zaidi: Serikali yaongeza kikokotoo pensheni ya wastaafu Tanzania


Mapato yatakayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa mujibu wa Dk Nchemba yanatarajiwa kuwa Sh1.36 trilioni, kiwango ambacho kimeongezeka kutoka Sh1.14 trilioni mwaka wa fedha unaoishia Juni mwaka huu.

“Serikali inakadiria kukopa Sh6.62 trilioni kutoka soko la ndani ambapo Sh4.02 trilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh2.60 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo,” amesema Dk Nchemba. 

Mbali na mikopo ya ndani, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inakadiria kukopa Sh2.99 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Katika mwaka huo wa fedha, misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inakadiriwa kuchangia Sh5.13 trilioni katika bajeti hiyo. 

Zaidi ya nusu ya bajeti kugharamia matumizi ya kawaida

Dk Nchemba amesema kuwa 34.6 trilioni ni matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 70 ya bajeti yote huku bajeti ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh14.76 trilioni sawa na asilimia 30.

Uchambuzi zaidi wa bajeti hiyo unabainisha kuwa Sh15.74 trilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya  ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu huku Sh11.77 trilioni zikitarajiwa kutumika kwa ajili ya mishahara ikiwemo ajira mpya pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi.

Related Post