Tanzania, Msumbiji kuongeza ushirikiano maeneo ya kimkakati

Fatuma Hussein 0925Hrs   Julai 02, 2024 Habari
  • Ni katika nyanja za kilimo, biashara, afya pamoja na ulinzi na usalama.
  • Zakubaliana kuongeza uwekezaji wa nchi na nchi kutoka 18 waliopo sasa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake itaendelea  kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Msumbiji katika nyanja za diplomasia, uchumi, ulinzi na usalama pamoja na siasa ili kuchochea ustawi wa mataifa hayo mawili.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wanahabari mara baada ya mazungumzo na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi leo Julai 2, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam amesema nchi ya Msumbiji sio tu nchi jirani ya Tanzania bali ni jirani wa mkakati, ndugu, na rafiki wa siku zote.

“Tulizungumza mahusiano yetu ya kibiashara tukasema kwamba kwa hadhi tuliyonayo kwenye mahusiano ya kisiasa bado biashara zetu ziko chini… tumezungumza kuongeza mahusiano ya kibiashara, kuongeza uwekezaji, tumesaini hapa leo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa ili kuchochea mahusiano ya kibiashara wamekubaliana kujenga kituo cha pamoja cha forodha cha Mtambaswala baada ya kubaini kuporomoka kwa biashara kutoka Dola milioni 57.8 sawa na Sh152.8 bilioni mwaka 2022 hadi Dola milioni 20.1 za Marekani sawa na Sh53.1 bilioni mwaka 2023.

“Tumekubaliana kuangalia sababu gani labda usalama ulizorota, biashara zilikuwa hazipitiki… lakini inawezekana pia baadhi ya transaction (miamala) zinazofanyika kibiashara hazipatikani officially (rasmi),” amebainisha Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema wamekubaliana kuongeza zaidi wawekezaji kwa mataifa hayo mawili kutoka Watanzania 16 waliowekeza hivi sasa nchini Msumbiji na kampuni mbili za Msumbiji zilizowekeza Tanzania.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi wakati wakizungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam.Picha l Ikulu

Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyoangaziwa na marais hao ni pamoja na kilimo, siasa, afya pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama.

Kwa upande wake Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, pamoja na kumshukuru Rais Samia kwa kuruhusu vikosi vya jeshi kushiriki oparesheni za kuimarisha amani Msumbiji amesisitiza nchi za Afrika kuendelea kuwa na umoja ili kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara hilo.

“Matatizo ya watu wa Afrika yanatakiwa kusuluhishwa na waafrika wenyewe, waafrika kwanza ndio walete majawabu,” amesema Rais Nyusi.

Rais wa Msumbiji yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kufuatia mualiko wa Rais Samia ambapo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara (saba saba) utakaofanyika Julai 3, 2024.

Ziara ya Rais Nyusi nchini itakuwa ya mwisho kama kiongozi wa juu wa wa Msumbiji kutokana na kuwa ukingoni kumaliza mihula miwili ya uongozi wake utaotamatika mwezi Oktoba 2024.

Awali viongozi hao pia walishuhudia uwekaji saini wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi, elimu.

Nyusi anatarajiwa kuondoka nchini Julai 04, 2024 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume baada ya kumaliza ziara binafsi visiwani Zanzibar.

Related Post