Serikali kushirikisha wadau, wasanii, viongozi wa dini kupambana na uchafuzi wa mazingira

Lucy Samson 0936Hrs   Juni 05, 2024 Habari
  • Dk Mpango asema ushirikiano huo utaokoa mazingira.
  • Watakaokaidi kutii sheria za mazingira kuchukuliwa hatua.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango amesema Serikali itashirikisha wananchi, viongozi wa dini, wasanii pamoja na wadau wa mazingira ili kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira nchini.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha siku ya mazingira duniani yaliyofanyika Juni 5, 2024 mkoani Dodoma amesema ushirikiano baina ya Serikali na wadau hao unaweza kuokoa mazingira.

“Ni muhimu kuimarisha ushirikiano wa dhati kati ya Serikali, asasi zisizo za kiserikali, sekta binafsi, wasanii wetu, taasisi za kidini, viongozi wa mila na wananchi kwa ujumla…kwa pamoja tunaweza kufanya mabadiliko makubwa, tena mabadiliko chanya ili kuokoa mazingira yetu,” amesema Dk Mpango.

Kauli ya Dk Mpango inakuja wakati Tanzania ikikabiliwa na uchafuzi wa mazingira ikiwemo utupaji taka, ukataji miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali ambapo husababisha mabadiliko ya tabia ya nchi.


Soma zaidi:Bei ya petroli dizeli yashuka kiduchu Tanzania


Bado takataka zinazagaa mitaani

Dk Mpango amesema kuwa Tanzania kwa sasa inazalisha tani milioni 7 za uchafu kila siku lakini nusu ya takataka hizo (milioni 3.5) hazikusanywi na kutupwa katika sehemu zinazotakiwa ikiwemo madampo huku nyingine zikizagaa mitaani.

Miongoni mwa takataka hizo ni plastiki ambazo wataalam wa mazingira wanazitaja kuwa hatari zaidi kwa maisha ya viumbe hai pamoja na binadamu.

“Na madhara ya taka za plastiki ni makubwa kiasi kwamba watafiti wa mazingira wanakadiria kuwa ifikapo 2050 idadi ya plastiki baharini itakuwa kubwa kuliko idadi ya samaki…taka hizo zinatengeneza sumu ambayo inaathiri viumbe maji na binadamu tunaotumia viumbe hivyo kwa ajili ya chakula,” ameongeza Dk Mapango.

Ili kukabiliana na tatizo hilo Dk Mapago amewataka wananchi kuzingatia mbinu bora za utupaji takataka katika madampo ya kisasa na kuhamasishana kutunza mazingira.

“Hakika hali hii haikubaliki na ni lazima watanzania tufanye jitihada kubwa zaidi kukusanya, kuchakata na kutupa taka katika katika maeneo mahususi na hasa madampo ya kisasa…

…Nawaomba sana watanzania kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayetupa taka hovyo na kuchafua mazingira yetu,” amesema Dk Mpango.

Awali Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ili kukabiliana na uchafuzi huo wa mazingira ni vyema viongozi kusimamia sheria za mazingira zilizopo na atakayekaidi achukuliwe hatua.

Related Post