Serikali kununua vichwa 22, mabehewa 1,490 kwa ajili ya SGR

Daniel Samson 0825Hrs   Julai 08, 2019 Habari
  • Mabehewa hayo yanajumuisha 1,430 ya mizigo na 60 ya abiria.
  • Safari ya kwanza ya majaribio ya treni ya wahandisi yazinduliwa.
  • Wakazi wa Arusha, Moshi kuanza kutumia usafiri wa treni Desemba hii.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Serikali imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni na mabehewa 1,490 yatakayotumika katika uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) ambayo ujenzi wake unaendelea.

Mabehewa hayo yanajumuisha 1,430 ya mizigo na 60 ya abiria yatakayotumika katika reli hiyo, inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkez ya Uturuki, kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi jijini Dodoma na baadaye hadi nchi za jirani za Rwanda, Burundi na Congo DRC.

Kamwelwe ameweka wazi mipango hiyo wakati akizindua safari ya kwanza ya majaribio ya treni ya wahandisi kwenye eneo la Soga lililopo Kibaha mkoani Pwani.

Amesema mpango wa sasa ni kuwa na Seti tano za treni za SGR zitakazokuwa na mabehewa nane ya abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha  sekta ya usafirishaji wa reli.

“Ndugu zangu Watanzania leo hii tumezindua majaribio ya njia ya reli yetu, hii ina maana kwamba tupo katika mipango ya kuhakikisha reli inakamilika kwa wakati, tumetembea kilomita 20 za majaribio, reli ni salama kabisa, haina kikwazo. 

“Sasa tumeanza mchakato wa kununua vichwa vya treni 22 na mabehewa yake 60 ya abiria na 1,430 ya mizigo,” amesema Waziri huyo.


Soma zaidi:


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema zoezi la majaribio ya awali ya treni ya wahandisi ni hatua muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha miundombinu ya reli hiyo.

Amesema zoezi hilo la awali limekuja kufuatia kukamilika kwa baadhi ya maeneo ya kupita treni kuanzia Soga Wilayani Kibaha Mkoani Pwani, kuelekea Morogoro na kuongeza kuwa treni rasmi kwa ajili ya kupita reli hiyo itawasili hivi karibuni.

Mpango wa sasa ni kuwa na Seti tano za treni za SGR zitakazokuwa na mabehewa nane ya abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha  sekta ya usafirishaji wa reli. Picha|Mtandao

Katika hatua nyingine, Kadogosa amesema TRC imeanza kukarabati njia ya Reli ya kati ya kutoka Dar Es Salaam mpaka Isaka wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga ili kuimarisha reli hiyo zoezi ambalo lilianza Juni mwaka huu na kutarajia kukamilika mwaka 2020.

Katika Ukarabati huo shirika hilo linatarajia kufunga njia za reli hiyo kwa saa 72 kwa wiki ikiwa kwa muda wa miezi mitano kuanzia Julai hadi Novemba 2019.

Kutokana na ukarabati huo ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), Serikali inatarajiwa kupata hasara ya Sh1.8 bilioni kutokana na kupungua kwa muda wa kufanya kazi. 

Amesema kwa treni za kawaida za mjini (Cummuter Train) za kutoka Kamata kwenda Ubungo na Pugu zitafanya kazi siku za Jumatatu hadi Ijumaa huku treni za kawaida (Ordinary Train) za kutoka Dar Es Salaam kwenda Kigoma, Mwanza na Mpanda zitafanya kazi siku za Jumatatu na Jumatano na treni za Deluxe kutoka Dar kwenda Kigoma zitakuwepo siku ya Jumanne pekee.

Amesema ukarabati mwingine wa njia ya reli kutoka Tanga kwenda  Arusha ulianza mapema mwaka huu ambapo njia hiyo itaanza kutumika mwezi Desemba mwaka huu.

“Ndugu zangu wa mikoa ya Kaskazini mtaanza kunufaika na usafiri wa treni ya Abiria kuanzia Desemba mwaka huu, yaani Sikukuu za Krismas na mwaka mpya mtaenda nyumbani na treni ya abiria ya TRC,” amesema Kadogosa.


Related Post