Serikali yazindua chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wa miaka 9 hadi 14

Mariam John 0713Hrs   Aprili 23, 2024 Afya & Maisha


  • Itasaidia kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi kabla hawajaanza ngono.
  • Chanjo hizo zinatolewa bure nchi nzima.

Mwanza:Tanzania imezindua chanjo ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 ambao hawajaanza kushiriki ngono.

Awali watoto hao walikuwa wakipata chanjo hiyo pale wanapofikisha umri wa miaka 14 hadi 18 jambo ililokuwa linachelewesha matibabu hayo muhimu. 

Kupitia chanjo hiyo iliyozinduliwa katika viwanja vya furahisha jijini Mwanza Aprili 23, 2024 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, watoto hao watapata dozi moja ya chanjo ya ugonjwa huo unaoshambulia via vya uzazi ambayo itatolewa bure nchini nzima.

Akizungumza na wakazi wa jiji la Mwanza, Waziri Ummy amesema  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na watafiti walibaini suluhisho la ugonjwa huo ni kuanza kuwakinga mapema watoto ambao hawajaanza kushiriki ngono.


Soma zaidi:33 wafariki kwa maafa ya mafuriko Rufiji, Morogoro


"Chanjo ambayo itaanza kutolea leo kwa mabinti itasaidia kukomesha ugonjwa wa saratani Tanzania na kwamba katika awamu hii hatutalazimika  kutoa dozi mbili kama ilivyokuwa inafanyika huko nyuma badala yake dozi moja ya saratani ya mlango wa kizazi itatosha kumkinga msichana na ugonjwa huo," amesema Waziri Ummy.

Akizungumzia zaidi kuhusu ugonjwa huo, Waziri Ummy amesema ugonjwa wa saratani unaongoza katika kuwatesa Watanzania ambapo katika kila wagonjwa 100 wa saratani, 23 ni wa saratani ya kizazi.

Waziri Ummy Mwalimu (katikati) akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa chanjo ya saratani ya kizazi kwa mabinti wenye umri kati ya miaka tisa hadi 14.Picha|Mariam John/Nukta Africa.

Asiliamia 11 ni wagonjwa wa  saratani ya mfumo wa chakula, asilimia 14 ni saratani ya matiti na tezi dume ikiwa na asilimia 8.9.

"Kuhudumia mgonjwa mmoja wa saratani kwa mwaka ni zaidi ya Sh8 wakati chanjo ya HPV dozi moja ni Dola za Marekani 3.5 sawa na Sh10,000 hivyo ni vyema wazazi wakaruhusu watoto wao waweze kupata chanjo hiyo ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo," amesema Waziri Ummy

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema takwimu za mwaka 2023  zinaonesha idadi ya wagonjwa waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi walikuwa 40 ,470, kati ya hao 1,510 walikuwa na dalili za awali huku  919 wakifanyiwa tiba mgando.

Aidha, amsema wanawake 90 sawa na asilimia 18 walithibitika kugundulika na tatizo hilo katika kipindi tajwa.

Related Post