Meli ya MV Mwanza yaanza majaribio Ziwa Victoria

Mariam John 1016Hrs   Machi 26, 2024 Habari
  • Ni jaribio la kwanza kati ya majaribio matatu yanayotakiwa kufanyika.
  • Majaribio hayo yataifanya meli hiyo kukamilika kwa asilimia 96.


Mwanza. Meli mpya ya MV Mwanza iliyokuwa inajengwa katika karakana ya Mwanza Kusini, imeanza kufanyiwa majaribio ya kiufundi kuona iwapo injini na mitambo mingine iliyowekwa ndani ya meli hiyo inafanya kazi kikamilifu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Erick Hamis aliyekuwa akizungumza wakati wa majaribio hayo amebainisha kuwa majaribio hayo ya siku tatu yataifanya meli hiyo kukamilika kwa asilimia 96.

Meli hiyo ambayo ni kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kukamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 20 na kati ya hayo matatu ni makubwa.

“Kwa mara ya kwanza toka meli hiyo ilipoanza kujengwa, leo meli hiyo inaanza kufanyiwa majaribio ya kiufundi kuona kama injini zilizowekwa, mitambo yote ya kuongozea meli na vifaa vingine kama vinafanya kazi vizuri,” amesema Hamis.

Muonekano wa meli ya MV Mwanza ikiwa kwenye bandari ya Mwanza Kusini kabla ya kuanza kufanyiwa majaribio. Pichal Mariam John/ Nukta Africa

Mkurugenzi huyo amesema katika majaribio hayo, kuna jopo la wataalamu zaidi ya 60 wakiwemo wakandarasi, wahandisi, wataalamu wa MSCL na wasambazaji wa mashine mbalimbali kutoka Marekani na China ambao wataangalia mashine zao zinavyofanya kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL, John Mbungo amesema ni wakati sasa kwa Wizara ya Viwanda kutumia fursa hiyo kwa kuwa na mikakati ya kuanza uzalishaji mitambo mingine.

“Tayari tumeshuhudia meli hii ikiundwa hapa hapa nchini, hivyo wataalamu wapo na tunaweza hata kuunda magari hapa hapa nchini,” amesema Mbungo

Related Post