Ahueni kwa wakazi wa Mtwara, Lindi kimbunga Kenneth kupungua nguvu

April 27, 2019 9:58 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

vipindi vya mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali vinaweza kujitokeza kufuatana na mchango wa mgandamizo huu katika kuvuta unyevunyevu kutoka magharibi kuelekea katika nchi yetu.Picha|Mtandao.


  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kimbunga hicho kimepungua nguvu na sasa kimebadilika na kuwa mgandamizo mdogo. 
  • Kwa sasa mgandamizo huo mdogo upo katika ardhi ya Msumbiji na hautarajiwi kutua katika ardhi ya Tanzania.
  • Lakini wakazi wa Mtwara na maeneo ya jirani wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya mvua kubwa inayoweza kunyesha tena. 

Dar es Salaam. Licha ya kimbunga Kenneth kupungua nguvu yake na kuwapatia ahueni wananchi wa Mtwara na Lindi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema bado wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya mvua kubwa inayoweza kunyesha siku za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, katika kipindi cha siku mbili zilizopita (Aprili 24 na 25, 2019)  kimbunga Kenneth kiliendelea kuimarika lakini iIlipofika saa 9 usiku wa kuamkia Aprili 26, 2019 kimbunga kilifika nchi kavu kaskazini mashariki mwa Msumbiji takribani kilometa 220 kusini mwa Mtwara.

Lakini nguvu ya kimbunga ilipungua zaidi jana ambapo kilibadilika kutoka kimbunga kamili na kuwa mgandamizo mdogo (Overland Depression “EX-KENNETH”).

“Matarajio ni kwamba mgandamizo mdogo (Overland Depression) “EX Kenneth” utaendelea kupungua nguvu huku kikisogea kuelekea kusini-mashariki mwa msumbiji ifikapo mchana wa tarehe 27 Aprili 2019,” inaeleza taarifa hiyo.

Hadi leo asubuhi, kimbunga hicho kimepungua nguvu ambapo kinasafiri kwa kilomita 40 kwa saa na kiko kilomita 297 kutoka pwani ya Mtwara.

MWENENDO WA KIMBUNGA KENETH KUSINI MASHARIKI MWA MSUMBIJI

               

Kwa sasa mgandamizo huo mdogo upo katika ardhi ya Msumbiji na hautarajiwi kutua katika ardhi ya Tanzania, lakini TMA inasema ni wazi kuwa siyo mbali sana na mpaka wa Tanzania, ni matarajio kuwa mifumo ya hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi yetu itaendelea kuendeshwa na mgandamizo huo. 

Kutokana na hali hiyo wananchi hasa wa mikoa ya Mtwara na Lindi wanaotumia bahari ya Hindi wameshauriwa kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na madhara yanayoweza kutokea wakati wakiendelea na shughuli zao.

“Aidha, vipindi vya mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali vinaweza kujitokeza kufuatana na mchango wa mgandamizo huu katika kuvuta unyevunyevu kutoka magharibi kuelekea katika nchi yetu,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya TMA.

TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa mgandamizo mdogo wa hewa uliopo kaskazini mashariki mwa nchi ya Msumbiji pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.


Soma zaidi:


Kutokana na mvua zinazoweza kunyesha katika siku tatu hadi nne zijazo, Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania umewataka raia wake waliopo nchini  kuchukua tahadhari wakati wakitembelea mikoa ya kusini kutokana mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya barabara.

“Unatakiwa kufuatilia taarifa za ndani na kimataifa za hali ya hewa za Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (World Meteorological Organisation) na mtendee kazi ushauri wa mamlaka za ndani,” inaeleza taarifa ya Ubalozi huo iliyotolewa jana. 

Kila mwaka takribani raia 75,000 wa Uingereza wanatembelea Tanzania.

Hata hivyo, Balozi wa Uingereza nchini Sarah Cooke ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa nchi yake inafuatilia kwa karibu mwenendo wa kimbunga Kenneth na kama madhara ya mvua yatatokea wako tayari kutoa msaada kama mamlaka husika zitahitaji. 

Hali ilivyo Msumbiji 

Baada ya kimbunga Kenneth kupiga jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji juzi jioni (Aprili 25, 2019) na sasa kimepungua kasi yake, Umoja wa Mataifa (UN) umechukua hatua ya kupeleka timu yake ili kusaidiana na serikali katika operesheni za usaidizi na usimamizi wa taarifa.

Tathmini ya awali ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) inaonyesha kuwa kimbunga Kenneth kimeathiri watu 16,776 , ambapo nyumba 2,934 zimebomoka kidogo huku 450 zimeharibiwa kabisa, madarasa 31 yameharibiwa pamoja na vituo vitatu vya afya. 

Msemaji wa Shirika la Hali  ya Hewa duniani (WMO), Claire Nullis wakati akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa (UN) amesema madhara ya kimbunga Kenneth yalikuwa ni madogo kwa kuwa kilipunguza kasi kabla ya  kufika ardhini na kilitua eneo la mashambani.

“Mamlaka za Msumbiji zilihamisha maelfu ya watu hatua ambayo ilipunguza madhara ya vifo. Na Tanzania, ambayo haijawahi kukumbwa na kimbunga cha kitropiki, ilitoa matangazo ya hadhari mapema kwa watu walio hatarini na maonyo hayo yanaendelea hadi leo hii, maonyo ya mafuriko na maporomoko ya udongo,” amesema Nullis.

Kimbunga Kenneth ni kimbunga cha pili kupiga Msumbiji ndani ya miezi miwili ambapo Machi 2019, eneo la kati mwa nchi hiyo lilikumbwa na kimbunga Idai kilicholeta madhara makubwa  kwa binadamu, mali na miundombinu.

Enable Notifications OK No thanks