Rais Samia aongeza dau ‘goli la mama’

Esau Ng'umbi 0630Hrs   Mei 18, 2023 Burudani
  • Sasa kutoa Sh20 milioni kwa kila goli la ushindi. 
  • Asema ndege ya Serikali itaipeleka na kuirudisha timu ya Yanga katika mchezo wa fainali.
  • Awaomba viongozi wa TFF kushirikiana kwa ukaribu na timu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameongeza motisha kwa Klabu ya Yanga kwa kila goli la ushindi litakalopatikana katika michezo ya kimataifa kutoka Sh10 milioni hadi Sh20 milioni.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa minara ya kurushia matangazo ya kampuni ya Azam Media amewaambia wahudhuriaji kuwa anaipongeza Yanga kwa kufuzu hatua ya fainali ya kombe la shirikisho na anaongeza dau ili kuwatia hamasa.

Nitumie jukwaa hili kuipongeza timu yetu ya Yanga, wamecheza kwenye mashindano yetu vizuri na niliwapa msukumo kidogo, sasa Yanga inakwenda kwenye Fainali, tunapokwenda kwenye fainali ni milioni 20 kwa kila goli la ushindi zaidi ya hapo Serikali itatoa ndege kuwapeleka katika mchezo wa fainali,” amesema Rais jijini Dar es Salaam.

Aidha Rais Samia amewaomba viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) kushirikiana na klabu hiyo kwa ukaribu ili kuwatia hamasa ya kupata ushindi kwani wanaiwakilisha nchi ya Tanzania kimataifa.

Awali Rais Samia alitangaza kutoa kiasi cha Sh5 milioni kwa kila goli la ushindi kwa vilabu vya Simba na Yanga ambavyo vilikuwa vinashiriki katika michuano ya kimataifa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL) pamoja na Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCF).

Klabu ya Simba iliondoshwa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya CAFCL ikiwa imevuna kiasi cha Sh45 milioni ya ‘goli la mama’ kutokana na magoli ya ushindi iliyopata.

Hata hivyo, mara baada ya Yanga kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali Rais aliongeza dau hadi Sh10 milioni kwa kila goli la ushindi na sasa ameongeza mpaka Sh20 milioni mara baada ya Klabu ya Yanga kufuzu kucheza fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

Yanga itacheza michezo yale miwili ya CAFCF na Timu ya ASM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza itachezwa Mei 28,2023 katika uwanja wa mkapa jijini Dar es Salaam na kurudiwa Juni 3 nchini Algeria.

Related Post