Utafanya nini elimu inapokutengenisha na mpenzi wako?

Rodgers George 0539Hrs   Februari 26, 2021 Burudani
  • Ni filamu inayomhusu binti Lara Jean ambaye malengo ya kuishi na mpenzi wake katika kipindi cha masomo ya chuo.
  • Ni baada ya kuona kuwa chuo kingine ndio kingemfaa zaidi.
  • Mpenzi wake halichukulii suala hilo kwa mtazamo chanya na hivyo kuivunja huba kati yao.

Dar es Salaam. Huwezi amini vitu ambavyo watu hufanya kwa ajili ya wapenzi wao. Wapo walio tayari kupigwa na risasi kwa ajili ya uhai wa wapenzi wao, wapo walio tayari kutembea umbali wa maili 1,000 na wale walio tayari kushinda njaa ili mpenzi wao ale.

Wewe umefanya nini kwa ajili ya mpenzi wako? Huenda ukawa katika njia panda kama alivyokuwa kwa Lara Jean ambaye ndoto yake ya kusoma chuo pamoja na mpenzi wake inakatishwa na uhalisia.

Kisa hiki kipo katika filamu ya “To All the Boys: Always and Forever” inayomsimulia binti Lara Jean na mpenzi wake Peter Kavinsky.

Wawili hao wana ndoto ya pamoja. Baada ya harakati za masomo kuwatenganisha hapa na pale, wanakubaliana kuwa inabidi wahakikishe wanaenda chuo kimoja na kwa sasa, ni chuo alichopo Kavinsky.

Hata  hivyo, hayo maamuzi siyo yake kwani kila chuo kina nafasi ya kuwachagua wanafunzi ambao kinaona wanafaa kuungana na chuo hicho.

Msemo wa “unapanga na yeye anapanga” anatimia kwake binti Jean ambaye maombi yake ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Stanford hayatimii na badala yeke, vyuo vitatu vinamkubali navyo ni Chuo Kikuu cha New York, Chuo Kikuu cha Berkeley na Chuo Kikuu cha California.


Soma zaidi:


Ni habari mbaya kwa Kavinsky ambaye tayari alikuwa ameshaandaa ratiba nzima ya maisha yao wakiwa chuoni ikiwemo kuturmbelea sehemu mbalimbali ikiwemo kusoma pamoja.

Kwa binti Jean, kukataliwa kwenda Stanford ni kupasuka kwa ndoto yake ya kuwa mwandishi wa vitabu, kuolewa na Kavinsky na kujenga naye familia.

Katika upande mwingine, mahaba kati ya Dr. Covey, baba yake Lara Jean na mwanamama Trina Rothschild yanapamba moto. Hilo huenda linampa viulizo binti Jean ambaye anaanza kuhisi kuwa huenda baba yake ameshamsahau mama yake.

Hakika ni vita ya kimawazo na hadi  hapa ilipofikia, huenda binti Jean akapasuka kichwa, huku analazimika kusoma maili nyingi mbali na mpenzi wake na sasa baba yake anahitaji kufunga ndoa ya pili.

Yapo hayo na zaidi ikiwemo kuachana kwa binti jean na Kavinsky, harusi isiyotegemewa na kufahamu chanzo cha kwanini baba Kavisnsky alimkimbia mwanaye.

Unaweza kuipata filamu hii kupitia mtandao wa Netflix endapo umelipia akaunti yako. Wikiendi ni muhimu kwa kuchangamsha mwili na akili yako. Itumie ipasavyo.

Pia, usisite kutupatia mapendekezo ya filamu unayohitaji tuisimulie na kupitia mitandao ya kijamii @Nukta Tanzania kupitia Faceboo, Twitter na Telegram pia, @nuktatz kupitia mtandao wa instagram.

Hadi wiki ijayo, kwaheri.

Kwa taarifa zaidi, usisite kutufikia kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram, Twitter na Facebook @NuktaTanzania 

Related Post