Umafia na wema: Filamu ya “Raya and the Last Dragon” inavyofundisha ujasiri, umoja

Rodgers George 0320Hrs   Aprili 23, 2021 Burudani
  • Inamhusu binti anayepambana na yasiyowezekana kumrudisha baba yake ambaye amegeuzwa na sanamu.
  • Ni baada wa makabila katika jamii yake kugawanywa na wivu, chuki na tamaa ya madaraka.
  • Tumaini la kumrudisha baba yake lipo lakini kulifikia, inahitaji aanze kujijenga kwanza.


Dar es Salaam. Kuna nadharia nyingi katika kutokuelewana kati ya kabila na kabila, nchi na nchi na hata mtu na mtu. Kwa baadhi sababu ni mali, kwa wengine ni maendeleo.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa huenda sababu kuu ni ubinafsi kwa maana ya kila mtu anataka kuwa juu ya mwenzake?

Katika ardhi ya Kumandra ambayo wakazi wake wamejaliwa vipaji mbalimbali, mambo ni shwari. Mwenye kucheza anacheza, mwenye kufua nguo anafua na hata mwenye kujifunza vitu anajifunza lakini wasichokijua ni kuwa siku inakuja ambapo yote hayo yatageuka kuwa historia.

Katika siku hiyo, wanavamiwa na viumbe giza vinavyoitwa Druun ambavyo vinabadilisha maisha ya wana Kumandra. Viumbe hao wakipita karibu na wewe, unabadilika kuwa sanamu.

Uzuri ni kuwa Wanakumandra wanalindwa na viumbe waitwao “Dragon” ambao wanasifa kama nyoka mkubwa mwenye miguu, nywele, mapembe na anayeweza kupaa.

Hata hivyo, juhudi za viumbe hao hazifui dafu na wanalazimika kuunganisha nguvu zao na kumuachia “dragon” mdogo zaidi anayejulikana kwa jina la Sisu ambaye maisha ya binadamu yanabaki mikononi mwake. 

Sisu anatumia nguvu za kaka na dada zake wote kuokoa wanadamu dhidi ya Druun lakini katika hatua hiyo, na yeye anatoweka na kuwaacha wanadamu wakiamini kuwa hawana ulinzi tena. Hata wakati akiondoka, anaacha jiwe la maajabu ambacho linaaminika kuwa na nguvu ya kufukuza viumbe vya Druun lakini linabaki katika uangalizi wa kabila moja na huo ndio mwanzo wa shida.

Raya ambaye aliaminishwa na baba yake kuwa kuna wema ndani ya kila mtu, anasalitiwa na mtu aliyedhani ni rafiki mpya. Picha|Creative Boom.

Matatizo yanaanza na mgawanyo wa Wanakumandra katika makabila matano ambayo ni kabila la Fang, Heart, Spine, Talon, na Tail ambayo majina hayo yanawakilisha sehemu za mwili wa kiumbe dragon.

Mgawanyo huo hauwafurahishi wote na zaidi ni Chifu Benja wa kabila la Heart ambaye anafanya kila analoliweza kurudisha jamii ya Wanakumandra kuwa moja. 

Benja ambaye ni mwangalizi wa jiwe lililoachwa na Sisu anamfunza Raya (bintiye) kuwa mwangalizi pia lakini huenda kosa lake ni kumhimiza binti huyo juu ya wema, jambo linalofanya wema kuelekezwa kwa mtu asiyefaa.

Wivu, tamaa ya madaraka na ubinasi unayafanya makabila mengine kufanya kila njia ya kumiliki jiwe hilo na siku ya kulipambania inapokuja, hakuna anayeondoka na jiwe hilo likiwa katika umbo moja. 

Katika filamu hiyo iliyotengenezwa kwa mfumo wa vikaragosi, kugombania jiwe hilo kunasababisha lipasuke na hapo ndipo Druun wanaporudi tena.

Kurudi kwa viumbe hao wa giza kunasababisha wengi kubakizwa kama sanamu akiwemo Chief Benja anayemwacha Raya peke yake na Wanakumandra wengine ambao hawana kipande cha jiwe la maajabu.


Soma zaidi:


Viangazi, vuli, chipuko na vipupwe vinapita lakini bado hakuna kilichobadilika. Waliokuwa sanamu bado ni sanamu na walioishi bado wapo katika hofu ya kimaisha wakitegemea maji kuwalinda dhidi ya Druun ambao hawapatani na maji. 

Wengine wameshasahau ndugu zao ambao ni sanamu lakini Raya, bado hajamsahau baba yake. Binti huyo anaanza safari ya kutafuta kipande kimoja baada ya kingine vya jiwe lililoachwa na Sisu ili alirudishie kuwa jiwe moja akiwa na matumaini, Dragon watarudi.

Katika safari hiyo anapambana na kabila moja baada ya lingine kukusanya jiwe hilo na anafanikiwa kumrudisha Sisu.

Je, kurudi kwa sisu ni matumaini ya Raya kumrudisha baba yake,  na je, dragon wengine ambao wamebaki sanamu nao watarudi?

Kuna njia moja tu ya kufahamu  majibu ya maswali hayo na ni kwa kuangalia filamu hiyo ambayo inaonyeshwa katika kumbi za kuangalizia filamu zikiwemo za Century Cinemax zilizopo katika maduka  makubwa (malls) jijini Dar es Salaam.

Raya and the Last Dragon inaweza kuwa ni fursa ya kumfundisha mtoto wako madhara ya ubinafsi, umuhimu wa umoja na matokeo ya kujiamini na pia kujiburudisha wakati wa kuhitimisha wiki yako. 

Kama filamu hiyo siyo fungu lako, zipo filamu zingine ikiwemo Vanquish, Mortal Combat na The Valt

Wiki ijayo tutakuwa na filamu gani? Endelea kubaki na Nukta Habari (www.nukta.co.tz)


Related Post