NIT kuanza kutoa mafunzo ya uhudumu wa ndege

Daniel Mwingira 0228Hrs   Agosti 13, 2018 Safari
  • Kozi hiyo ya miezi mitatu inatarajiwa kuanza Septemba 17 mwaka huu ikihusisha watu waliofaulu vyema mtihani wa kumaliza kidato cha nne (CSEE).
  • Watakaomba kusoma kozi hiyo hawatakiwi kuwa na urefu unaopungua Sentimeta 160.

Dar es salaam. Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) sasa imegeukia katika sekta ya usafiri wa anga baada ya kuanza kutoa kozi ya mafunzo ya uhudumu wa ndege nchini. NIT ni maarufu kwa mafunzo ya udereva wa magari, masuala ya uchukuzi na ugavi. 

Hatua hiyo imekuja baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kuiruhusu NIT kuanza kufundisha kozi za wahudumu wa ndege (Cabin Crew and recurrence courses) zinazotarajiwa kuanza Septemba 17 mwaka huu.

Katika tangazo lililotolewa leo (Agosti 13, 2018) kwenye vyombo vya habari, NIT inaeleza kuwa watu wanaotaka kusoma kozi hiyo wanatakiwa kuwa na angalau Cheti cha Kuhitimu Elimu ya Sekondari (CSEE) wakifaulu vyema masomo Jiografia,  Historia, Kiswahili na Kingereza au cheti cha masuala ya utalii na usafiri wa anga.

Hata hivyo, siyo wote wenye sifa hizo za elimu watapata nafasi ya kujiunga na chuo hicho baada ya NIT kuweka ukomo wa urefu usiopungua Sentimeta 160 na umri wa zaidi ya miaka 18.



Kozi hiyo ya miezi mitatu inakuja wakati ushindani katika sekta ya usafiri wa anga nchini ukiongezeka kwa kasi hasa baada uamuzi wa Serikali ya Rais John Magufuli wa kufufua Shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania) ambalo hadi sasa lina ndege tano ikiwemo kubwa ya kisasa aina ya Boeing 787-8 Dream Liner. 

Kuanza kutolewa kwa kozi hiyo katika chuo hicho kunaongeza wigo wa fursa za masomo na idadi ya vyuo vinavyotoa mafunzo hayo ambayo awali yalikuwa yakitolewa pia na Chuo cha Air Tanzania. Mafunzo ya aina hiyo hutoa fursa kwa vijana wa kitanzania wanaopenda kufanya kazi katika mashirika ya ndege ndani na nje ya nchi.

Moja ya majengo ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Jijini Dar es Salaam. Chuo hicho kimeanza kutoa kozi za uhudumu wa ndege ndege. Picha|Mtandao.

Related Post