Magoroto: Pepo ya Tanzania iliyojificha wilaya Muheza

Rodgers George 0930Hrs   Septemba 06, 2018 Safari
  • Awali msitu wa Magoroto ulikuwa mashamba ya Watawala wa Kijerumani na baadaye ukahifadhiwa kama sehemu muhimu yenye uoto wa asili.
  • Upekee wake ni kuwepo kwa Ziwa lililotengenezwa na binadamu lenye viumbe mbalimbali wakiwemo samaki.
  • Msitu huo unatumika kama sehemu ya utunzaji wa mazingira kutokana na uwezo wake wa kuhifadhi uoto wa asili ambao haupatikani katika maeneo mengine nchini.

Dar es Salaam. Kila binadamu mwenye uhai anayefanya kazi kikamilifu anahitaji mapumziko. Siyo usingizi tu wa siku moja lakini muda mrefu ambao atautumia katika mazingira tulivu kurejesha mawazo, akili na mwili katika hali ya kawaida.

Tafsiri ya mapumziko inatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Wengine mapumziko ni kuacha shughuli za kiofisi au biashara na kutulia na familia nyumbani wakati wa likizo. Lakini wengine ni wakati wa kuwatembelea ndugu au kwenda kwa wazazi kijijini.

Wapo wengine mapumziko ni  sehemu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii ikiwa ni sehemu ya kubadilisha mazingira waliyoyazoea na kujifunza vitu vipya.

Basi kama wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda utalii, sehemu sahihi ya kwenda mwishoni mwa mwaka huu ni katika msitu wa Magoroto uliopo wilaya ya Muheza,  kilomita 37 toka katika Jijini la Tanga.

Msitu huo wenye ukubwa wa ekari 591 na ziwa la maji masafi, ulifunguliwa mwaka 1896 na Watalawa wa Kijerumani kama shamba la kwanza la kibiashara Afrika Mashariki.  Kwa mara ya kwanza shamba hilo lililima zao la mpira baada ya kushindwa kulima kahawa na chai na baadaye kulimwa michikichi mwaka 1921.

Eneo hilo lilichukuliwa na wazawa “kundi la Amboni” mwaka 1940 na kilimo cha michikichi kilisitishwa baada ya kuwepo ushindani kati ya Malaysia na Indonesia. Baada ya hapo, Msitu wa Magoroto ulihifadhiwa mpaka leo kwa kuzingatia upekee na uzuri wake.

Pamoja na kupakana na msitu wa Mlinga, Magoroto  inatengeneza vipande vya milima ya Usambara ambayo inafahamika kwa uzuri na upekee wa uoto wa asili. Unafahamika zaidi kwa uwepo wa ndege wa kipekee ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Chama cha Uhifadhi Wanyamapori wanahusika katika uhifadhi wa misitu hiyo nchini.

Mogoroto ni kivutio cha utalii siyo Muheza pekee bali kwa mtu yeyote mwenye nia ya kutembelea eneo hilo kutokanana hali yake ya hewa kuwa nzuri huku ikiambatana na mandhari nzuri ya chini ya milima.

Ziwa Magoroto ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaotembelea eneo hilo. Picha| Picbear

Eneo hili humpatia mtu muonekano mzuri kutoka bonde la Muheza hadi bahari ya Hindi na pia kumfurahisha mtu na mimea adimu na ndege au matembezi katika mashamba ya mawese ya zamani. Pia kujifunza juu ya viungo asilia kama pilipili, karafuu, mdalasini, chai, vanila pamoja na vingine vingi vyenye umuhimu au kuogelea katika ziwa zuri la Magoroto.

Kinachowapa mshawasha wengi kutembelea Magoroto ni  picha za baadhi ya watu ambao wamewahi kufika eneo hilo lilipo Kaskazini mwa Tanzania ambapo anaona ni sehemu muafaka kutuliza akili. 

Mkazi wa Dar es Salaam, Ally Mwanyiro ni miongoni mwa watu ambao utalii ni sehemu ya maisha yake.

“Ninapenda mazingira asilia kwahiyo Magoroto ilikuwa ni mahali sahihi kuona kijani inayovutia.” Aliifahamu Magoroto kupitia rafiki yake ambaye familia yake inamiliki eneo hilo.

Mwanyiro ambaye kitaaluma ni Mhandisi wa kompyuta alitembelea Mgoroto Februari mwaka huu ambapo kilichomvutia ni uasili wa eneo hilo akifananisha na paradiso ya duniani. 

“Inatuliza kusikia ndege wakiimba na upepo ukivuma taratibu, kupanda milima ya Usambara, kuogelea kwenye ziwa lenye ukubwa wa kati lilotengenezwa na binadamu na kuota moto  nyakati za usiku,” amesema Mwanyiro.


 Zinazohusiana:


                         

Mandhari ya misitu ya Magoroto. Video| Jeremiah Mchechu


Kwa nini Magoroto?

Meneja wa Msitu wa Magoroto, Jeremiah Mchechu ameiambia Nukta kuwa Mtalii atakayefika eneo hilo ataweza kupanda milima, kutembea, kuendesha baiskeli, kuogelea kwenye Ziwa Magoroto, kuvua samaki, kuwaona ndege, kutembea msituni, kutembelea kavazi na eneo la viungo. Pia utapata fursa ya kucheza michezo mbalimbali na muziki nyakati za usiku.

Hata hivyo, vizuri vina gharama, kufika kwako Magoroto kutakufanya utoboe kidogo mfuko ili kufurahia vivutio vingi. Gharama zake kwa siku moja ni kiasi kisichopungua 100,000 ambapo inahusisha gharama za baiskeli kwa ajili ya kutembea milimani, chakula cha siku nzima, na shughuli zote zitakazofanyika huko.

Kwa watoto walio chini ya miaka mitano ni bure na miaka sita hadi 13 atalipia nusu bei ya mtu mzima. Watalii kutoka nje ya nchi wao watalipia Dola za Marekani 75 (Sh170,000) tu kwa siku moja.

Magoroto ni sehemu ya kipekee kwa utalii hivyo ni vema ukajiandaa na kuweka oda yako mapema ikizingatiwa kwamba eneo hilo linaweza kuhudumia watu 30 hadi 40 kwa siku ili kuhakikisha mazingira ya asili ya eneo hilo hayaharibiwi.

“Wageni kutoka nje ya nchi bado hawafahamu sana kuhusu msitu huu,” amesema Mchechu na kuongeza kuwa wanaendelea na juhudi za kutangaza ili kuongeza shughuli za utalii na kuwa sehemu ya kuchangia pato la Taifa.

 

Related Post