Jinsi ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza

Mariam John 1212Hrs   Machi 21, 2024 Afya & Maisha
  • Ni pamoja na kuepuka tabia bwete a ulaji usiofaa.
  • Wataalamu wa afya washauri kuzingatia ulaji sahihi wa vyakula ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta.


Mwanza. Wakati dunia ikiendelea kushuhudia wimbi la ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Hospitali ya Nyamagana, Dk.Sarah Mwendi anasema kubadili mtindo wa maisha ni miongoni mwa njia za kuu za kukabiliana na magonjwa hayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaainisha magonjwa yasiyoambukiza kuwa ni saratani, magonjwa ya moyo, kisukari pamoja na magonjwa ya mfumo wa upumuaji ambayo huwaathiri sana watu wenye vipato vya chini na vya kati.

Magonjwa hayo husababisha vifo vya watu takribani milioni 41 kila mwaka sawa na asilimia 76 ya vifo vyote vinavyotokea duniani.

Dk. Mwendi ameiambia Nukta habari kuwa miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia magonjwa hayo ni pamoja na mfumo usiofaa wa maisha ambao unahusisha tabia bwete na ulaji usiofaa.

“Ninavyoongelea ulaji mbovu, ninaongelea ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi kama chips, piza…ni muhimu watu wakazingatia ulaji wa mlo kamili ambao umekusanya virutubisho vyote,” amesema Dk. Mwendi.

Sababu nyingine ambazo husababisha magonjwa hayo ni uvutaji wa sigara na tumbaku, matumizi ya vilevi, pamoja na athari za uchafuzi wa hewa.


Soma zaidi:Magonjwa ya moyo bado tishio duniani


Jinsi ya kuepuka magonjwa yasiyoambukiza

Ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dtk. Mwendi amewashauri wananchi  kuzingatia ulaji sahihi wa vyakula ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta hali ambayo itasaidia kupunguza magonjwa hayo.

Pia wametakiwa kuzingatia ufanyaji wa mazoezi kwa wingi ili kupunguza magonjwa hayo ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu kwa kuwa maradhi hayo yanatumia gharama kubwa katika kuyatibu.

Kwa upande wa kituo anachofanyia kazi Dk. Mwendi amebainisha kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wanaoripoti katika hospitali hiyo hubainika kuwa na magonjwa hayo hususani presha na sukari huku kundi linaloathirika zaidi ni wanawake.

“Wanawake kwa maana ya kwamba ndio watu wanaojitokeza kwa wingi kwenda kuchunguza afya zao tofauti na wanaume ambao hata kama anashida hiyo huchukulia kawaida au wakati mwingine kupata mawazo yasiyo sahihi kutoka kwa marafiki,” amesema Dk.Mwendi

Kwa mujibu wa Dk. Mwendi  asilimia 15 ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo husumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza, huku wengi wakisumbuliwa na presha na kisukari.

Baadhi ya wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo kupata matibabu ya magonjwa hayo yasiyoambukiza wamesema pamoja na kupatiwa huduma zote mhimu lakini wanakumbana na changamoto ya gharama kubwa za matibabu na kuiomba Serikali ingalie namna ya kuwapunguzia.

“Tunahudumiwa vizuri, lakini changamoto tunayokumbana nayo ni gharama za matibabu kuwa kubwa, na unaweza kupatiwa dawa aina moja nyingine unaelekezwa kwenda kununua sehemu nyingine hivyo tunaomba Serikali itusaidie dawa ziweze kupatikana hospitali,” amesema Mary Minga mkazi wa Mahina.

Related Post