Magonjwa ya moyo bado tishio duniani

Husna Miraj 1138Hrs   Septemba 29, 2023 Afya & Maisha
  • Watu zaidi ya milioni 17 wanapoteza maisha duniani kutokana na magonjwa ya moyo kila mwaka.
  • Tanzania ina wagonjwa wa moyo milioni 3.4.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya moyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema zaidi ya watu  milioni 17 dunaini kote hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya moyo.

Shirika hilo limebainisha kuwa magonjwa ya moyo ikiwemo kiharusi (stoke) na mshtuko wa moyo (heart attack) ni magonjwa yanayoongoza kwa idadi kubwa ya vifo kuliko magonjwa mengine yasiyoambukiza.

“Magonjwa ya moyo husababisha vifo vingi vya magonjwa yasiyoambukiza (NCD) milioni 17.9 kila mwaka, ikifuatiwa na saratani (milioni 9.3), magonjwa ya mfumo wa upumuaji (milioni 4.1), na kisukari milioni 1.5...

…Makundi haya manne ya magonjwa yanachangia zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya mapema vya magonjwa yasiyoambukiza,” limesema Shirika hilo.


Soma zaidi : Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani


Wakati hayo yakiendelea, tafiti iliyofanywa na Chama cha Madaktari Bingwa wa moyo Tanzania (TCS) na kuchapishwa na tovuti ya ‘National Library Medicine’ ya nchini Marekani inaonyesha kuwa asilimia 13 ya watanzania walipoteza maisha kutokana na magonjwa hayo.

Utafiti huo uliochapishwa mwaka 2020 unafafanua kuwa takwimu hizo za idadi ya vifo nchini Tanzania ni hadi  kufikia mwaka 2017.



Wagonjwa wa moyo waongezeka

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyekuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo Septemba 29,2023 jijini Dar es Salaam amesema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo yanazidi kuongezeka nchini.

“Takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya moyo na shinikizo la Juu la damu pekee kutoka wagonjwa milioni 2.5 Mwaka 2017 hadi wagonjwa milioni 3.4 Mwaka 2022,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri huyo amesema magonjwa ya moyo ikiwemo ugonjwa wa Kiharusi yanaweza kuzuilika ikiwa wananchi watachukua hatua za haraka kukabiliana nao.


Soma zaidi : Unakunywa gongo, chang’aa au kachasu? Fahamu uhusiano wake na saratani


“Sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya Kiharusi ni pamoja na kutozingatia ulaji unaofaa ambapo kwa nchi yetu inaonesha asilimia tatu tu ya watu wazima wanatumia kiasi cha wastani wa kutosha cha matunda na mboga mboga”. Amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema idadi ya watu wazima wanaofanya mazoezi ni imeongezeka ukilinganisha na vijana huku akiwasihi kutenga muda zaidi wa kufanya mazoezi.


Related Post