Fahamu chanzo, jinsi ya kuondoa rangi nyeusi kwapani

Lucy Samson 0130Hrs   Mei 04, 2023 Afya & Maisha
  • Wataalamu wa afya wasema fangasi na uchafu ndio visababishi vikubwa vya weusi kwapani.
  • Usafi na kuepuka matumizi ya vifaa vya kunyolea visivyo sahihi ni mbinu ya kuepukana na tatizo hilo.

Dar es Salaam. Weusi kwapani? Ndio.  Ni jambo la aibu  kwa baadhi ya watu na hawapendi kulizungumzia suala hili hadharani. 

Baadhi yao hulazimika kuvaa nguo zenye mikono mirefu kwa kuepuka sehemu hizo kuonekana.

“Kwa sisi wanawake weusi kwapani unatutesa, unashindwa hata kuvaa nguo za kuogelea kwa amani ukihofia kuaibika endapo watu wakikuona,” anasema Anaheri Richard mkufunzi wa kuogelea (swim coach) jijini Dar Es Salaam.

Ikiwa wewe ni mmoja wa wahanga wa tatizo hili makala hii ni kwa ajili yako ambapo tutaangazia chanzo na jinsi ya kuondoa weusi kwapani.


Fangasi ndio chanzo cha weusi makwapani

Daktari Zabron Mbatiya kutoka Hospitali ya Kairuki ya jijini Dar es Salaam anasema chanzo kikubwa cha weusi kwapani ni maambukizi ya fangasi wa ngozi wanaopendelea kukaa sehemu zenye joto na unyevu unyevu.

“Tatizo hili husababishwa na fangasi aina ya ‘candida’ ambao huota kwenye makwapa, chini ya matiti, sehemu ya ndani ya mapaja na ndani ya  mashavu ya uke,” amesema Dk Mbatiya.

Fangasi hao hujishikiza kwenye vitundu vya vinyweleo na kusababisha miwasho ambapo kadri mtu anavyojikuna ndivyo weusi unavyoongezeka katika sehemu hizo.

Mbali na uwepo wa fangasi, Meshack Mhalila, mtaalamu wa afya wa kujitegemea kutoka mkoani Mbeya anasema kunyoa kwa vifaa visivyo sahihi kama viwembe butu pamoja na uchafu huchangia makwapa kuwa meusi.


Zinazohusiana


Mtaalamu huyo amesema baadhi ya watu hawajisafishi ipasavyo na kusababisha mlundikano wa uchafu sugu ambao mwisho hutengeneza rangi nyeusi.

“Wengine hawajisafishi vizuri, hayo maeneo hayasuguliwi kabisa hapo lazima kuwe na rangi nyeusi… pia wale wanaovaa nguo za kubana kwa muda mrefu wanaweza kupata tatizo hilo,” anasema Mhalila.

Sambamba na hayo wataalamu hao wa afya wamesema matumizi yaliyokithiri ya vidhibiti harufu (vipodozi) makwapani na sehemu nyingine za mwili yanachangia sehemu hizo kuwa nyeusi kutokana na wingi wa kemikali zilizopo.


Fanya haya kuepukana na weusi kwapani

Licha ya kwamba tatizo hilo linatibika ikiwa utatembelea vituo vya afya na kutumia dawa, zipo mbinu zitakazokusaidia kuepukana nalo.

Wataalamu wa afya wanasema ili kuepukana na weusi kwapani njia ya kwanza ni kuhakikisha usafi wa sehemu hizo mara kwa mara.

“Sehemu ambazo zina uchafu ndipo fangasi wanapenda kukaa hivyo ukijisafisha na kujiweka safi unapunguza uwezekano wa fangasi kuzaliana na kusababisha weusi,” amesema Dk Mbatiya.

Kunyoa kwapani kwa vifaa sahihi ni miongoni mwa njia itakayokusaidia kupunguza weusi kwapani. Picha | Popsugar.

Kunyoa kwapani kwa vifaa sahihi

Baadhi ya vifaa vinavyotumika kunyolea huwa ndio kisababishi cha weusi kwapani. Wataalamu hao wa afya wanasema kutumia vifaa bora vya kunyolea kunaweza kusaidia.

“Watu wananyoa kwa kiwembe, hali lazima iwapate hususani akiwa amenyoa kwa muda mrefu,” amesema Mhalila.


Epuka matumizi yaliyokithiri ya vidhibiti harufu (vipodozi)

Matumizi yaliyokithiri ya vipodozi vinavyodhibiti harufu maarufu kama ‘deodorant na spray’ yanayoweza kusababisha ngozi ya kwapa kuwa nyeusi.

Mhalila anasema vipodozi hivyo huzuia mchakato wa utoaji taka mwili kwa njia ya jasho na kusabisha maeneo hayo kuwa meusi.

“Vipodozi vyenye viambata vya ‘aluminium salt’ husababisha seli za ngozi kufa ndio maana unakuta maeneo hayo ni meusi ikimaanisha kuwa maeneo hayo hakuna uhai,” ameongeza Mhalila.


Related Post