Hakuna kulala: Rais Samia afanya mabadiliko makubwa vigogo taasisi za Serikali

April 5, 2021 7:11 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amewaondoa baadhi yao kwenye nafasi zao na kuweka wapya.
  • Baadhi ya waliondolewa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko na bosi wa TCRA, James Kilaba.
  • Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ateuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali. 

Dar es Salaam. Huenda Jumatatu ya Pasaka isiwe njema kwa baadhi ya vigogo wa taasisi za Serikali akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko ambaye anachunguzwa baada ya kuondolewa katika nafasi zao jana. 

Rais, Samia Suluhu Hassan jana Aprili 4, 2021 amefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa wizara, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali huku baadhi wakiondolewa na kuhamishwa katika nafasi walizokuwa wanatumikia awali. 

Rais Samia katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, amewaondoa waliokuwa wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali na nafasi zao zimechukuliwa na watu wengine, ikiwa ni mabadiliko ya mwanzo aliyoyafanya tangu aingie madarakani Machi 19 katika taasisi za Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko ambaye alisimamishwa kazi hivi karibuni kupisha uchunguzi ameondolewa na nafasi yake amechukuliwa na Erick Hamis.

Kakoko, ambaye alithibitishwa kuwa bosi wa TPA mwaka 2018 baada ya kuwa kaimu wa taasisi hiyo alisimamishwa kazi na Rais Samia mwezi uliopita baada ya kubainika ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni kwenye taasisi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Hamis alikuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanznaia  (MSCL) ambayo inasimamia shughuli za usafirishaji kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. 

Kiongozi mkuu huyo wa nchi pia ameigusa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo amemteua Alphayo Kidata kuwa kamishna mkuu wa mamlaka hiyo akichukua nafasi ya Edwin Mhede ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu Juni 2019. 

Unaweza kusema Kidata ana bahati ya mtende kwa sababu hii ni mara ya pili kuteuliwa kuwa kamishna mkuu wa TRA. Mara ya kwanza Kidata aliteuliwa na Hayati Magufuli mwaka 2016 akichukua nafasi ya Dk Philip Mpango ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Kwa sasa, Dk Mpango ni Makamu wa Rais wa Tanzania katika Serikali ya awamu ya sita.Hata hivyo, Marchi 25 2017 Hayati Dk Magufuli  alimteua Kidata kuwa Katibu Mkuu Ikulu na baadaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan ambapo Novemba 2018 uteuzi wake ulitenguliwa na alivuliwa ubalozi na kurejeshwa nchini. 

Tangu wakati huo, Kidato hakushika wadhifa wowote na hakuwahi kuonekana hadharani, mpaka alivyoibuliwa na Rais Samia jana na kuteuliwa tena kuwa Kamishna Mkuu wa TRA. 

Rais wa sita wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Picha| Steven Mgenya

Panga lapita pia TCRA na TPDC

Mama Samia hakuziacha salama taasisi nyingine nyeti za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambapo Mkurugenzi wake Mkuu James Kilaba ameondolewa katika nafasi hiyo.

Nafasi yake imechukuliwa na Dk Jabir Kuwe ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA). 

Dk Kuwe atakuwa na kibarua kigumu cha kushughulikia suala la vifurushi vya simu ambavyo hivi karibuni vimezua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii baada ya gharama zake kuongezeka hasa za intaneti, jambo ambalo limelalamikiwa na watu wengi kuwa zinawaumiza. 

Naye bosi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James  Mataragio, kibarua chake kimeota nyasi baada ya Mwesiga Richard kuchukua nafasi yake. Mabadiliko mengine yaliyofanywa na Mama Samia ni kumteua Kaimu Mkeyenge kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) akichukua nafasi ya Emmanuel Ndomba.

Masha Mshomba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi za jamii (NSSF) ambapo amechukua nafasi ya William Erio. Kabla ya uteuzi huo, Mshomba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Mshomba atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha mafao ya wastaafu yanatolewa wakati ikizingatiwa kuwa kumekuwa na malalamiko mbalimbali ya watu kuzungushwa na kucheleweshewa mafao yao baada ya kustaafu.


Soma zaidi:


Rais Samia ambaye aliteuliwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi mwaka huu, amemteua Gerald Kusaya kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya akichukua nafasi ya Rogers Sianga ambaye amedumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2017. 

Kabla ya uteuzi huo, Kusaya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye nafasi yake imechukuliwa na Andrew Massawe.

Pia katika uteuzi huo ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu tangu Rais Samia adokeze Aprili mosi mwaka huu alipokuwa anawaapisha mawaziri aliowateua jijini Dodoma, amemteua Dk Aifello Sichwale kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Profesa Abel Makubi.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Dk Hussein Abbasi.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Abbasi alikuwa akihudumu katika nafasi mbli ya Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamduni, Sanaa na Michezo. 

Enable Notifications OK No thanks