Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
- Kabla ya kuwa Rais alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania tangu mwaka 2015.
- Alishika nafasi mbalimbali Serikalini na ndani ya chama cha CCM.
- Anakuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania.
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiwa katika maombolezo ya kitaifa ya kifo cha Rais John Magufuli, Tanzania imeandika historia ya aina yake tangu kupata uhuru mwaka 1961.
Historia hiyo ni kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameapishwa leo Machi 19, 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kushika nafsi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa nchi, Mama Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania tangu mwaka 2015 chini ya uongozi wa awamu ya tano wa Dk Magufuli.
Lakini leo cheo chake kimebadilika na sasa ni rasmi Rais wa sita wa Tanzania ambaye ataongoza nchi hadi mwaka 2025.
Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa rais aliyepo madarakani akifariki dunia hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika badala yake makamu wa rais ataapishwa kuwa rais kwa kipindi kilichosalia.
Kwa mujibu wa katiba hiyo ibara ya 37 (5), baada ya Samia kuapishwa atashauriana na chama anachotoka ambacho ni CCM kisha atamteua mtu atakayekuwa makamu wa Rais.
Safari ya Mama Samia kuwa rais wa Tanzania ilikuwa ndefu kwa sababu imehusisha elimu, uzoefu wa uongozi alioupata tangu akiwa mdogo.
Sasa Mama Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Tanzania. Picha| The Star.
Huyu ndiye Rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia alizaliwa visiwani Zanzibar Januari 27, 1960 na alipata elimu ya msingi kuanzia mwaka 1966 na kumaliza mwaka 1972 huku akisoma elimu hiyo katika shule tofauti tofauti: Shule ya Msingi Ziwani (Pemba), Mahonda na Chwaka za visiwani Unguja.
Rais huyo mwenye miaka 61 aliendelea na safari ya elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Ngambo na Lumumba zilizopo Unguja na mwaka 1977 alijiunga na Chuo cha Utawala wa Fedha Zanzibar (ZIFA) alipochukua masomo ya takwimu.
Soma zaidi:
- Serikali: Taratibu mazishi ya Rais Magufuli kujulikana Machi 19
- Wamachinga, wajasirimali waeleza Magufuli alivyowainua Mwanza
- Viongozi, jumuiya za kimataifa wazungumzia watakavyomkumbuka Rais Magufuli
Safari ya kitaaluma na utumishi wa umma
Baada ya kumaliza masomo, safari yake ya ajira ilianza katika Wizara ya Mipango na Maendeleo.
Mwaka 1986 alijiunga na masomo ya juu ya Utawala wa umma katika Chuo cha Usimamizi wa Maendeleo (IDM) ambacho kwa sasa kinafahamika kama Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo Mkoani Morogoro.
Baada ya kuhitimu Mzumbe alipata fursa ya kusoma nje ya nchi. Mama Samia alijiunga na Chuo cha Utawala wa Umma kilichopo Lahore nchini Pakistan.
Mwaka 1991 alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Viongozi kilichopo Hyderabad nchini India kwa ngazi ya cheti.
Baada ya kurejea nchini Tanzania, mwaka 1992 aliajiriwa katika mradi uliowezeshwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Kutokana na kupenda kusoma, Rais Samia alirudi tena masomoni katika Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo London nchini Uingereza kuchukua Stashahada ya Uzamili katika masuala ya uchumi.
Mwaka 2004 hadi 2005, aliendelea na masomo yake akichukua Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Uchumi wa Jamii iliyotolewa na programu shirikishi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire cha Uingereza.
Kabla ya kushika nafsi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa nchi, Mama Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania tangu mwaka 2015 chini ya uongozi wa awamu ya tano wa Dk Magufuli. Picha| The Citizen.
Safari ya kisiasa
Baada ya safari ndefu ya masomo na shughuli za kikazi, Mama Samia liingia kwenye uwanja wa kisiasa, licha ya kuwa alikuwa mwanachama wa muda mrefu wa CCM.
Mwaka 2000, Rais Samia alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kuteuliwa kuwa Waziri na Rais Amani Karume akiwa mwanamke pekee aliyeshikilia nyadhfa ya juu zaidi katika Baraza la Mawaziri.
Mwaka 2005, aliwania Ubunge katika jimbo la Makunduchi akishinda kwa zaidi ya asilimia 80. Safari yake ilibadilika mwaka 2014 ambapo Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Muungano.
Mwaka huo huo wa 2014 aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililopewa kazi ya kuandika Katiba mpya ya nchi.
Ilipofika mwaka 2015, Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Hayati Dk John Magufuli alimchagua kama mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Baada ya Hayati Dk Magufuli kushinda Urais mwaka 2015, Samia aliapishwa kama Makamu wa Rais wa Tanzania akiwa ni Makamu wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania.
Aliendelea na wadhifa huo katika kipindi cha pili cha urais wa Dk Magufuli kabla hajafariki dunia Machi 17, 2021.
Sasa Mama Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Tanzania.