Bei vifurushi vya simu: Ni maumivu zaidi ya ilivyotarajiwa

April 2, 2021 12:14 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Watumiaji wa simu walalamika kupanda kwa gharama za vifurushi vya simu kuliko matarajio waliyokuwa nayo.
  • Suala hilo limezua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi wakitaka Serikali kuingilia kati.
  • Mjadala umekuja wakati kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi kuanza kutumika leo. 

Dar es Salaam. Watumiaji wa huduma za intaneti na simu nchini Tanzania Aprili 2 wameamka na bei mpya za vifurushi ambazo wengi wanaona ni maumivu zaidi ya walivyotarajia kiasi cha kuwaongezea gharama za maisha.

 Mabadiliko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Sehemu kubwa ya huduma za vifurushi imebadilishwa huku kwenye intaneti kukiwa na maumivu zaidi.

Gharama hizo mpya zimeibua mjadala mpana kwenye jamii hususan kwenye mitandao ya kijamii huku watu wengi wakilalamika kuwa walitarajia kuwa uamuzi wa Serikali kudhibiti huduma hizo ungeleta nafuu lakini si hivyo. 

Kanuni hizo ambazo zilitungwa na TCRA zilitangazwa mwezi uliopita zimeanza kutumika rasmi leo Aprili 2, 2021 ambapo zina lengo la kutatua changamoto na kero ya kuwepo kwa malalamiko ya makato yasiyo sahihi ya gharama za matumizi ya vifurushi vya simu za mkononi Tanzania.

Miongozi mwa malalamiko hayo ni pamoja na gharama za juu za vifurushi na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara. Kanuni hizo zinasimamia vifurushi vya dakika za kupiga miongoni mwa mitandao ya nchini, bando ya intaneti na meseji. 

Jana Aprili mosi, mitandao yote ya simu ikiwemo ya Tigo, Zantel, Vodacom, Airtel, TTCL iliwataarifu watumiaji wake juu ya mabadiliko hayo kama zinavyoelekeza kanuni hizo.

Hoja kubwa iliyopo ni kuminywa kwa vifurushi hivyo kuliko hata ilivyokuwa awali wakati wanatoa malalamiko hayo.

Mabadiliko ya vifurushi vya simu yaibua mjadala kila kona Tanzania. Picha| Mtandao.

Kilio kila kona

Mathalan,  katika mtandao wa Tigo, kifurushi cha Saizi Yako kilikuwa kikitoa GB1 kwa Sh 1,000 ambayo ingeweza kutumika kwa siku tatu lakini sasa, kifurushi hicho kinatoza Sh1,000 inayoambatana na MB300 za kutumika ndani ya saa 24 huku Sh10,000 inakuwezesha kupata GB4.5 za intaneti. 

Mfanyabiashara mkoani Dar es Salaam Ivan Phares ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa intaneti ina mchango mkubwa katika maendeleo ya mtu binafsi na kupandisha gharama ya virushi ni kupunguza kasi ya maendeleo hayo.

Phares, mtumiaji wa mtandao wa TTCL, kwa sasa anapata MB980 kwa Sh1,000 ambayo ni chini ikilinganishwa na zamani alipokuwa akipata zaidi ya GB 1.

“Kwa sasa naona TTCL ina unafuu kuliko mitandao yote. Lakini mwaka mmoja uliopita nilikuwa napata vifurushi vizuri zaidi,” amesema Phares.

Kwa mfanyabiashara huyo, ulimwengu wa sasa unategemea teknolojia na pale kampuni za simu zinapoanza kuweka ugumu katika upatikanaji wa teknolojia (intaneti) hiyo ni kutaka kuua maendeleo ya watu.

Mtumiaji wa mtandao wa Tigo, Elisha Samson kutoka Mbeya amesema amechoka na suala hilo kwa sababu anatumia fedha nyingi kupata vifurushi vya data ambavyo havidumu muda mrefu.

“Sina jinsi inabidi nipunguze matumizi ya intaneti ili niokoe fedha kwa sababu ziwezi tena kumudu gharama zake. Nitapitwa na mengi ya mtandaoni lakini maisha yataendelea kibishi tu,” Samson ameiambia Nukta.


Soma zaidi:


“Kilichofanywa na kampuni za simu ni sawa”

Mtaalam wa masuala mawasiliano pepe, Mhandisi Charles Kobelo amesema yeye anaamini watoa huduma wamezifuata kanuni za TCRA kama ilivyokuwa imetangazwa na yanayooneka kwa sasa ndiyo matokeo ya kanuni zilizowekwa.

“Mitandao ya simu wanapata leseni ya kufanya kazi kutoka TCRA wakienda kinyume na maagizo ni faini au kufungiwa. Nahisi wamefata. Hawawezi kuingia kwenye “risk” wanayojua sheria inasema nini. Pia siyo mtandao mmoja umefanya hivyo, ni yote ikimaanisha ni agizo,” amesema Kobelo ambaye ni mtaalam wa teknolojia.

Hata hivyo, mdau huyo amesema ni kawaida kwa kampuni za mawasiliano kuanzisha biashara zikiwa na ofa kedekede na bando za vifurushi zinazovutia ili kupata wateja wengi. Pale lengo lao linapotimia, ofa hizo zinakuwa zimefikia kikomo chake.

“Mitandao yote wananunua data (intaneti) kwa Ttcl, inamaanisha Ttcl wao ndiyo waamuzi wa kiasi gani mtumiaji wa mwisho atalipa kwa sababu wakiwauzia kwa gharama kubwa hayo makampuni pia watauza kwa gharama kubwa hawawezi fanya biashara bila faida,” amesema Mhandisi Kobelo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.

Wengine wanahoji kwanini kampuni za simu zipandishe bei ya vifurushi wakati TCRA imetoa kanuni ambazo zinalenga kusimamia vifurushi hivyo visiwaumize watumiaji wa simu?

Mtumiaji wa Facebook, Makanga Mwana wa Siwale ameandika kwenye mtandao huo kuwa, “ Tigo baada ya watu kulalamika sana juu ya gharama kubwa za vifurushi vyenu vya intaneti, mmeamua kuongeza gharama mara dufu bila shaka mpo kwa ajili ya kuwakomoa Watanzania wanyonge. Bei za vifurushi zinapanda tu.”

Ombi la watumiaji hao wa simu za mkononi Tanzania ni kupunguza gharama za vifurushi au kurudi katika mfumo wa vifurushi vya awali ambavyo vilikuwa ahueni kuliko vya sasa. 

“Hakuna hata heri hapa mnatuumiza tu bora hata vifurushi vingebaki kama awali tu,” ameandika Precious Tz katika mtandao wa Facebook wakati akijibu ujumbe wa Tigo kuwatakia wateja wake  Ijumaa Kuu njema. 

Waziri wa Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile mwishoni mwaka 2020 aliigiza TCRA kufanyia kazi malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na wananchi dhidi ya kampuni za simu, kuhusu kukatwa au kuibiwa fedha zao kwenye gharama za vifurushi.

Dk Ndugulile alisema mamlaka hiyo inatakiwa kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto hizo.

Enable Notifications OK No thanks