Kuna nini bandarini: Rais Samia aanza na bosi wa TPA

March 28, 2021 11:02 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia asema ripoti ya CAG imebaini uwepo wa ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni. 
  • Amsimamisha bosi wa TPA kupisha uchunguzi zaidi.

Dar es Salaam. Deusdedit Kakoko, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni moja ya watu wenye bahati mbaya zaidi mwezi huu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza asimamishwe kazi mara moja kupisha uchunguzi wa ubadhirifu dhidi ya taasisi hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kakoko, ambaye alithibitishwa kuwa bosi wa TPA mwaka 2018 baada ya kuwa kaimu wa taasisi hiyo, anakuwa kiongozi wa awali kabisa kusimamishwa kazi na Rais Samia ambaye alitwaa madaraka Machi 19 baada ya kufariki aliyekuwa Rais wa Tanzania Dk John Magufuli. 

Katika hotuba yake leo Machi 28, 2021 wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mwaka 2019/20 Ikulu jijini Dodoma, Rais Samia amesema baada ya kupitia ripoti ya CAG imebainika kuna ubadhirifu mkubwa uliofanywa na mamlaka hiyo ya bandari.

“Naomba Takukuru hii ni ‘special’ kazi (kazi maalum), mjishughulishe pale. Najua Waziri Mkuu aliunda kamati na wakafanya uchunguzi kidogo pale na mambo yaliyotoka hatua chache zilichukuliwa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia baada ya kupokea ripot ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kwa mwaka wa fedha 2019/20. Picha/Msemaji Mkuu wa Serikali.

Katika ripoti aliyokabidhiwa jana jioni, Rais Samia amesema imebainika uwepo wa ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni. 

“Wakati Waziri Mkuu amefanya ukaguzi waliosimamishwa ni hawa wa chini huku naomba mara moja nitoe agizo la kumsimamisha mkurugenzi mkuu wa bandari. Halafu uchunguzi uendelee,” amesema kiongozi huyo wa juu wa nchi.

Kusimamishwa kwa Kakoko na uchunguzi mwingine uliokuwa umefanywa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa mwaka jana ni dalili kuwa bado hali ilikuwa haijatengemaa ndani ya TPA ambayo ilikuwa ni moja ya maeneo ambayo Hayati Dk Magufuli alikuwa akiyaangizia kwa karibu katika kuchochea mabadiliko ya kiufanisi.

Uchunguzi ulioagizwa na Rais Samia huenda ukasaidia kufahamu mengi yanayoendelea katika taasisi hiyo miaka iliwahi kuwa na historia ya changamoto za kiufanisi. 

Hayati Dk Magufuli alifanya ziara kadhaa zikiwemo za kustukiza katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni muhimu kwa biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kutoa maagizo ya kuimarisha ukaguzi wa mizigo na ukusanyaji wa mapato.

Katika hotuba yake leo, Rais Samia amesema ataendelea kusimamia ipasavyo matumizi na mapato ya Serikali.

“Niwahakikishie kwenye mambo haya ya matumizi na makusanyo ya fedha za Serikali nitasimama imara. Lakini pia kwenye masuala ya rushwa pia nitasimama imara,” amesema Rais Samia.

Enable Notifications OK No thanks