Fursa nyingine ya mafunzo ya nishati jadidifu kwa wanahabari Tanzania

October 11, 2019 5:35 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yanalenga kumsaidia mwanahabari kuzalisha habari za nishati kwa ubora wa hali ya juu na zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
  • Wanahabari watakaochaguliwa pia watakuwa na fursa ya kushiriki katika kambi ya wanahabari na darasa maalum la wataalam.
  • Mwisho wa kutuma maombi ni Oktoba 18, 2019. 

Dar es Salaam. Wanahabari wenye kiu ya kujifunza kuhusu nishati jadidifu Tanzania na fursa zake, huenda ni wakati wao sahihi kupata maarifa hayo na kuongeza wigo wa kuripoti habari hizo zenye mchango mkubwa katika maendeleo nchini. 

Shirika lisilo la kiserikali la Hivos Afrika Mashariki (Hivos East Africa) kwa kushirikiana na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wameandaa mafunzo maalum ya wanahabari kwa vitendo katika masuala ya nishati jadidifu (Renewable energy reporting).

Mafunzo hayo ya miezi sita, yanayotarajiwa kuanza Desemba, 2019, yanalenga kumsaidia mwanahabari kuzalisha habari za nishati kwa ubora wa hali ya juu na zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na kwa vyombo habari husika. 

Nishati jadidifu huzalishwa na vyanzo vya asili kama jua, upepo, maji, jotoridi na mawimbi. 

Kimsingi vyanzo hivi ni endelevu na ni rafiki kwa mazingira ukilinganisha na kuni, makaa ya mawe, mafuta na gesi. 

Mafunzo hayo pia yatawawezesha wanahabari kutokutegemea maudhui kutoka kwenye makampuni na mashirika pekee bali yatafungua mlango wa kufahamu njia mpya za kidijitali za kuandika habari zikiwemo za takwimu (Data Journalism) na uthibitishaji habari (Fact Checking).

Wanahabari watakaochaguliwa pia watakuwa na fursa ya kushiriki katika kambi maalum ya wanahabari jijini Dodoma (Bootcamp) na kushiriki darasa (masterclass) jijini Dar es Salaam litakalowakutanisha na wataalam mbalimbali wa habari na nishati. 

Pia, watapata fursa ya kutembelea miradi inayoendeshwa na nishati jadidifu katika maeneo mbalimbali nchini ili kujifunza kwa vitendo na kuongeza uwezo wao wa kuripoti katika sekta ya nishati. 

Hii ni mara ya pili kwa Hivos na Nukta Afrika kuandaa mafunzo kama hayo, ambapo mwaka huu wameungana na JET kufanikisha programu hiyo mahususi kwa ajili ya kuongeza uelewa na matumizi ya nishati jadidifu kwa jamii. Picha|Mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen ameiambia www.nukta.co.tz kuwa mafunzo hayo yana muhimu kwa wanahabari na vyombo vyao vya habari ukizingatia kuwa maudhui ya nishati jadidifu yanafaa katika nyanja zote za kihabari iwe masuala ya kibiashara, uchumi, kijamii, siasa, teknolojia na mazingira.

“Mbali na kuzalisha maudhui, vyombo vya habari vinavyoripoti habari za nishati jadidifu mara kwa mara kama matumizi ya nishati ya umemejua ni rahisi sana kupata matangazo ya aina hiyo kwa kuwa watangazaji wana uhakika kuwa kuna kundi kubwa la watumiaji wa bidhaa na huduma hizo.

“Hii ni fursa adimu kwa wanahabari wa Tanzania baada ya kuadimika kwa mafunzo ya namna hii nchini na fedha za kwenda kufanya habari vijijini,” ameongeza.

Dausen amewataka wanahabari kuchangamkia fursa hiyo kwani itawapa fursa ya kujifunza kwa undani juu ya sekta ya nishati, ikizingatiwa kuwa kwa sasa mafunzo kama hayo yamekuwa adimu kwa vyombo vya habari. 

“Kwa sasa ni vigumu sana kuona vyombo vya habari vikiwa na bajeti maalum ya mafunzo ya ndani kutokana na changamoto za kifedha zinazotokana na kuporomoka kwa mapato ya matangazo. Hivyo, nawasihi wanahabari wenzangu kuomba na kuwa makini wakati wanajaza fomu ili waweze kuchaguliwa.

“Umakini katika kujibu maswali husika na utayari wa kujifunza masuala ya nishati jadidifu ni moja ya masuala makuu ambayo majaji wataangalia kipindi hiki,” amesema. 

Ili kuhakikisha maarifa yatakayopatikana katika mafunzo hayo yanatumika ipasavyo, wanahabari watapatiwa ruzuku  ya kuwawezesha kufanya uchunguzi wa kihabari katika maeneo watakayochagua na kuzalisha habari zilizofanyiwa utafiti wa kina kuhusu nishati jadidifu.

Usaili wa washiriki utazingatia wasifu, motisha waliyonayo, usawa wa kijinsia, taaluma, aina ya chombo cha habari na eneo unalotokea hapa nchini. 

Tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni Oktoba 18, 2019. Bonyesha hapa kuipata fomu ya maombi

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amewahamasisha wanahabari kujitokeza kwa wingi kupata fursa ya mafunzo hayo kwa sababu yanakusudia kuwaongezea uelewa na weledi wa kuripoti kwa ufasaha habari za nishati.  

“JET na waandaaji tumejipanga vizuri kuona kwamba tunachagua washiriki ambao watafanya kazi ya kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu nishati jadidifu. 

“Tutahakikisha wataalamu mbalimbali wanashirikishwa wakati wa mafunzo ili kutoa elimu kwa waandishi ambayo itasaidia kufanikisha malengo ya mradi katika kuleta tija kwa wanahabari na sekta ya nishati,” amesema Chikomo. 

Nukta Africa, Hivos zaongeza ushirika

Hii ni mara ya pili kwa Hivos na Nukta Afrika kuandaa mafunzo kama hayo, ambapo mwaka huu wameungana na JET kufanikisha programu hiyo mahususi kwa ajili ya kuongeza uelewa na matumizi ya nishati jadidifu kwa jamii.

Mwaka jana, waliandaa mafunzo yaliyowashirikisha wanahabari 20 ambao walipata fursa ya kushiriki tamasha maalum la nishati kwa wanahabari (Energy Change Safari for Journalists) kwa siku tano mkoani Arusha. 

Pia walipata mafunzo maalum Jijini Dar es Salaam na baadaye walienda katika maeneo mbalimbali nchini ili kufanya uchunguzi na kuandaa habari za kina kuhusu maendeleo ya nishati jadidifu. 

Mmoja wa wanahabari kutoka gazeti la Nipashe aliyeshiriki mafunzo hayo, Jeniffer Julius ameiambia www.nukta.co.tz kuwa mafunzo hayo yamemuwezesha kupiga hatua kubwa katika kuripoti habari za nishati na kumfungulia fursa za kushiriki makongamano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi. 

“Nilipata fursa ya kwenda Ghana na Ujerumani kuhudhuria mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Julius akibainisha kuwa ameongeza uelewa wa sekta ya nishati na fursa zake. 

Naye Sauli Gilliard kutoka gazeti la Daily News aliyeshiriki mafunzo hayo amesema yamemuongezea uwezo wa kuona fursa za kupata mawazo ya habari kila anaposafiri hasa katika maeneo yenye miradi ya nishati. 

“Kwanza kabisa ninapoenda mahali au nishati inapotajwa…Najiuliza is renewable/sustainable? (ni jadidifu au endelevu?),” amesema Gilliard ambaye baada ya mafunzo hayo aliandika habari kuhusu faida za kiuchumi zinazotokana na matumizi ya taa za barabarani zinazotumia umemejua mkoani Lindi. 

Amesema habari alizoandika wakati huo anakusudia kuziwasilisha katika mashindano mbalimbali ili kujipatia tuzo ya umahiri katika kuripoti habari za nishati jadidifu. 

Enable Notifications OK No thanks