CAG : Wagonjwa wa afya akili hawatambuliwi Tanzania

Lucy Samson 0847Hrs   Machi 28, 2024 Afya & Maisha
  • Asema Wizara ya Afya nchini Tanzania ilikuwa na mapungufu katika kuwabaini wagonjwa hao mwaka 2022/2023.
  • Apendekeza kuongezwa kwa bajeti na wataalamu wa afya ya akili.

Dar es Salaam. Huenda suala la afya ya akili likapata msukumo mpya nchini Tanzania kwa kuongezwa wataalamu wake, jambo litakalosaidia kuiponya jamii na masaibu yatokanayo, mara baada ya ripoti kubainisha suala hilo limekuwa likipuuziwa na mamlaka za afya.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini mapungufu katika sekta ya jamii hususan katika kushughulikia magonjwa ya afya ya akili.

Afya ya akili ni miongoni mwa maeneo yanayopigiwa chapuo zaidi na wadau wa afya nchini na duniani kutokana na kuongezeka kwa waathirika wa tatizo hilo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema mwaka 2019 karibu watu 270 duniani kote walikuwa na matatizo ya afya ya akili huku wengi wakionesha dalili kama wasiwasi, msongo wa mawazo na unyogefu.


Soma zaidi:ATCL yapata hasara ya Sh56.6 bilioni mwaka 2022-23


Wakati dunia ikiendelea na mapambano ya ugonjwa huo ripoti ya CAG kwa mwaka 2022/2023 imebaini mapungufu yaliyofaywa na Wizara ya Afya nchini Tanzania katika kuwabaini wagonjwa wa afya ya akili katika ngazi ya jamii.

“Utambuzi wa wagonjwa wa afya ya akili haufanywi kwa ufanisi katika ngazi ya jamii, utambuzi unaofanywa unalenga waathirika wa dawa za kulevya, wazee walemavu na watoto walio katika mazingira magumu na wale wanaoishi katika mazingira magumu…

…Hii inasababishwa na ukosefu wa fedha na wataalamu wa ustawi wa jamii katika ngazi ya vijiji na mitaa,” amesema CAG Charles Kichere aliyekuwa akiwasilisha ripoti ya ukaguzi leo Machi 28, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam.

CAG amebainisha kuwa huduma za kupata ushauri wa kisaikolojia kwa wagonjwa wa afya akili nchini haijapewa kipaumbele kwa kuwa haijajumuishwa katika sera za afya wala kutengewa bajeti maalum kama inavyofanyika katika magonjwa mengine ya kuambukizwa na yasiyoambukiza.


Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Afya ummy Mwalimu aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/2024, Serikali ilifanya kongamano moja tu la afya ya akili lililokutanisha wananchi na wadau 8,300.

Hata hivyo, jitihada hizo hazitoshi kukabiliana na tatizo la afya ya akili ambalo mara nyingi madhara yake huonekana pale linapotokea tatizo au maafa.

Mathalan maporomoko ya matope mkoani Manyara katika wilaya za Katesh na Hanang yaliyomfanya Rais Samia kuagiza timu ya wanasaikolojia kuwahudumia wananchi mkoani humo.

CAG atoa mapendekezo kuboresha mapambano dhidi ya afya ya akili

Ili kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya afya ya akili CAG ameshauri Serikali kupitia wizara ya afya  kutenga fedha kwa ajili ya kushughulikia magonjwa hayo katika ngazi ya jamii pia kuajiri wataalamu zaidi wa afya ya akili.

“Kuhakikisha huduma za kisaikolojia ziinapatikana kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya jamii, pia kuanzisha vituo vya utengeamo katika mikoa yote na wataalamu watakao saidia wagonjwa kupona,” amesema CAG Kichere.

Related Post