ATCL yapata hasara ya Sh56.6 bilioni mwaka 2022-23

Lucy Samson 0644Hrs   Machi 28, 2024 Habari
  • Hasara yaongezeka kwa asilimia 61 licha ya ruzuku ya Sh31.5 bilioni iliyotolewa.
  • CAG atoa mapendekezo ya kuimarisha ukusanyaji mapato katika mashirika hayo.


Dar es Salaam. Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilipata hasara ya Sh56.6 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/2023 iliyoongezeka kwa asilimia 61 kulinganisha na mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa za CAG , shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa hasara tangu kuanzishwa kwake licha ya juhudi za Serikali kulifufua kwa kununua ndege mpya na kutoa ruzuku.

Ikiwa ni sehemu ya maboresho na uwezeshaji wa ATCL katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilinunua ndege mpya ikiwemo ndege kubwa ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba mizigo ya tani 56.

Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali Charles Kichere aliyekuwa akizungumza  leo Machi 28, 2024 wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka 2022/2023 amesema hasara ya ATCL imeongezekakwa asilimia 61 licha ya ruzuku ya Sh31.5 bilioni iliyotolewa na Serikali.

“Hasara ya ATCL imetokea licha ya kupokea ruzuku ya Sh 31.55 bilioni kutoka serikalini na kurudisha bilioni  9.71 ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato,” amesema Kichere. 


Zinazohusiana:Hasara ya ATCL yapungua, Rais Samia aanika madudu mapya


Kwa mujibu wa mkaguzi huyo, hasara ya ATCL imeongezeka kwa asilimia 61 kulinganisha hasara ya Sh35.2 bilioni iliyorekodiwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mwaka 2021/2022 hasara iliyotengenezwa na shirika hilo ilipungua kwa asilimia 2.7 kulinganisha hasara ya Sh36.2 bilioni  iliyoripotiwa mwaka 2020/2021 jambo lililotoa matumaini chanya katika sekta hiyo muhimu nchini.

Baadhi ya wadau wamekuwa wakitoa maoni ya namna ya kuboresha utendaji wa shirika hilo akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Zitto kabwe aliyeshauri mifumo ya uendeshaji wa shirika hilo kuundwa upya kwa mifumo ya uendeshaji.


Hasara zaidi kwa mashirika mengine

Ripoti ya CAG imebainisha hasara katika mashirika mengine ya umma ikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni Tanzu ya Mafuta (TanOil ) na Shirika la Posta Tanzania.

TTCL ilitengeneza hasara ya milioni 894, iliyopungua  kwa asilimia 94 kulinganisha na hasara ya bilioni 19.23 iliyorikodiwa mwaka 2022/2023.

“Shirika limetengeneza hasara hii ya mwaka licha ya kupokea ruzuku ya Sh4.55 bilioni kutoka Serikalini na wamerejesha Sh 4.4 bilioni ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato yao kwa mwaka wa fedha 2022/2023,” amebainisha CAG Kichere.

Kwa upande wa shirika la TRC, CAG amebainisha kuwa limepata hasara ya Sh100.7 bilioni iliyopungua kwa asilimia 47.32 kulinganisha Sh190.01 bilioni licha ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh32.81 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Aidha, TanOil imepata hasara ya Sh76.56 bilioni likiwa ni ongezeko la Sh68.72 bilioni  kutoka Sh7.84 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/2023 huku Shirika la Posta Tanzania likipata hasara ya Sh1.34 iliyochangiwa na kupungua kwa gharama za EMS na gharama za uendeshaji.


Mapendekezo ya CAG

Ili kuimarisha mashirika ya umma yaweze kutengeneza faida CAG amependekeza kuchukuliwa kwa hatua za makusudi kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuundamikakati ya kufanya mageuzi katika uwekezaji usio na ufanisi.

Mbali na mapendekezo hayo ameitaka Serikali kusimamia uendeshaji  wa mashirika hayo huku wakifanya uchaguzi wa wafanyakazi wenye uwezo na ufanisi.

“Serikali inapaswa kuhakikisha mashirika yanaendeheswa na wafanyakazi wenye weredi, ubunifu na uwezo unaohitajika ili kuongeza ufanisi wa kubiashara…Serikali Inapaswa kuimarisha uangalizi wa taasisi na kwa kuteua wajumbe wa bodi wenye utaalaumu na maarifa katika sekta husika,” amesema CAG Kichere.

Related Post