Ahueni ya foleni: Magari yaruhusiwa kuanza kupita ‘Flyover’ ya Tazara Dar

Nuzulack Dausen 0743Hrs   Septemba 15, 2018 Habari

Magari yakipita kwenye barabara ya juu baada ya Serikali kuanza kuyaruhusu kupita kuelekea uzinduzi rasmi Oktoba 2018. Picha: Msemaji Mkuu wa Serikali. 

  • Barabara hiyo ya juu ni ya kwanza kujengwa nchini.
  • Matumizi ya barabara hiyo yatasaidia kuokoa asilimia 80 ya muda ambao hutumika kusafiri kutoka Posta mjini kwenda ‘Airport’.

Dar es Salaam. Foleni katika barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam sasa huenda ikapungua kwa kiwango kikubwa baada ya Serikali kuruhusu kutumika kwa barabara ya juu (flyover) katika eneo la Tazara.

Matumizi ya barabara hiyo yaliyoanza leo asubuhi (Septemba 15, 2018) yatafanya magari yanayotoka katika maeneo ya katikati ya Jiji ya Posta na Kariakoo kupitiliza bila kupanga foleni kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ulishawahi kueleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa flyover hiyo, iliyojengwa na kampuni ya Japan ya Sumitomo Mitsui, kutasaidia kupunguza msongamano wa magari kutoka Posta hadi ‘Airport’ kwa asilimia 80.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi ameeleza katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Serikali imeamua kuruhusu kutumika kwa barabara hiyo ya juu ya kwanza kujengwa nchini kuelekea uzinduzi rasmi mapema mwezi ujao.

Makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela hufahamika kuwa moja ya maeneo ya foleni kubwa ya magari jijini Dar es Salaam hasa nyakati za asubuhi na jioni.

Sasa flyover hiyo, yenye daraja lenye urefu wa mita 425, itafungua upande wa barabara ya Nyerere na kuruhusu vyombo vya moto vinavyotoka Gongo la Mboto kwenda mjini kupita moja kwa moja bila kusubiri foleni.  

Mara baada ya kuruhusu magari kupita kwenye flyover hiyo yenye thamani ya takriban Sh100 bilioni, uchambuzi wa taarifa za moja kwa moja za foleni za mtandao wa Google uliofanywa na Nukta umebaini kuwa hakukuwa tena na foleni katika eneo hilo ukiachana na magari yanayotokea barabara ya Nyerere na kuingia Mandela.  

Hali ya foleni katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere baada ya Serikali kuruhusu magari kupita katika barabara ya juu. Picha| Google Maps.

Hali halisi ya foleni ambayo huwepo katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere katika siku za Jumamosi muda kama ambao Serikali iliruhusu magari kupita juu ya flyover.

Related Post