Rais Samia uso kwa uso na bosi mpya wa Benki ya Dunia

July 8, 2022 11:54 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Kufanya mazungumzo na Rais Samia na Mwinyi wa Zanzibar wiki ijayo.
  • Atafanya ziara ya siku mbili baada ya kuanza majukumu mapya.
  • Lengo ni kukagua maendeleo ya miradi wanayoifadhili.

Dar es salaam. Rais mpya wa Benki ya Dunia ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika Dk Victoria Kwakwa anatarajia kufanya ziara nchini Tanzania wiki ijayo ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan na Hussein Mwinyi wa Zanzibar.

Ziara hiyo ya siku mbili itakuwa Julai 11-12 mwaka huu ambapo ni ziara yake ya kwanza ya kikazi nchini Tanzania tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo akichukua nafasi ya  Dk Hafez Ghanem ambaye amestaafu. 

Dk Kwakwa anatarajiwa kukutana  na Rais Samia, Rais Mwinyi pamoja na mawaziri, maafisa wa Serikali na washirika wa maendeleo kutoka taasisi za kiraia na binafsi. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia leo Julai 8, Dk Kwakwa atakutana na wanufaika wa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo kupitia Dirisha la Maendeleo la Kimataifa (IDA) ambalo kwa sasa linafadhili miradi 24 ya kitaifa yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.1 sawa na Sh14 trilioni.


Soma zaidi


Sekta ambazo zinafadhiliwa na mradi huo ni usafiri kwa asilimia 32.5, elimu (asilimia 26.7), maji (asilimia 9.7), maendeleo vijijini (asilimia 10.1) na ulinzi wa jamii kwa asilimia 7.6.

Sekta nyingine ni nishati asilimia 5.4, mazingira (asilimia 2.5), maendeleo ya kidijitali (asilimia 2.5) na Serikali pamoja na takwimu kwa asilimia tatu.

Mtaalamu huyo wa uchumi na maendeleo mwenye uzoefu wa miaka 30 ameongoza benki hiyo kushirikiana na mataifa 26 ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, ambapo amesimamia oparesheni zaidi ya 313 zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 58 sawa na Sh135 trilioni za Tanzania 

Maono ya Dk Kwakwa ni kuwa na ukanda imara na unaostahimili  mabadiliko ya kiuchumi na jamii zenye ustawi ambapo raia wote hasa wanawake, watoto na vijana wanafurahia usawa wa fursa.

Vipaumbele vyake

Chini ya uongozi wake Benki ya Dunia itaendelea kutoa msaada katika mataifa yanayokumbana na changamoto mbalimbali za kiuchumi ikiwemo madhara ya janga la UVIKO-19, chakula, mafuta pamoja na mfumuko wa bei.

Baadhi ya Vipaumbele vyake ni kuimarisha sekta binafsi, kufanya mabadiliko ya kiuchumi, kuimarisha rasilimali watu, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuimarisha kilimo na usalama wa chakula pamoja na kuimarisha miundombinu bila kusahau usawa wa kijinsia.

Kabla ya kuteuliwa kwake Julai Mosi mwaka huu, Dk Kwakwa alikuwa Makamu Rais wa Mipango na Mikakati ya Biashara akifanya kazi kwa ukaribu na Mkurugenzi wa oparesheni wa Benki ya Dunia ili kuhakikisha malengo lengwa yanafikiwa.

Amewahi pia kuwa makamu wa rais wa benki hiyo katika ukanda wa Asia Mashariki na Pasifiki kati ya Aprili 2016 mpaka Agosti 2021.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW