Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?

August 25, 2018 11:00 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakulima kuuza kahawa kwenye mnada wa pamoja.
  • Biashara haramu ya mipakani yafungwa kudhibiti mapato ya Serikali.
  • Wadau waishauri Serikali kutegua kitendawili cha bei ya kahawa kuwanufaisha wakulima.

Dar es Salaam. Huenda wakulima wa kahawa wakaanza kufaidika na bei ya soko baada ya Serikali kutengeneza mfumo wa manunuzi wa zao hilo ambao utawaleta pamoja vyama vya ushirika na kampuni ili kudhibiti biashara haramu ya zao hilo inayofanyika mipakani.

Mfumo huo ni ule wa kuuza kahawa kwenye mnada wa pamoja unaofanyika kila mwaka ambapo wakulima hawaruhusiwi tena kuuza kahawa kwa watu binafsi wanaowafuata mashambani au kupeleka nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa. 

Uamuzi huo wa serikali umeanza kutumika Julai mwaka huu (2018) na unafanyika chini ya usimamizi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ambayo imepewa jukumu la kupanga bei kulingana na gharama za uzalishaji na upatikanaji wa soko.  

Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amesema kampuni zenye kibali zinatakiwa kununua na kuuza kahawa kupitia vyama vya ushirika ili kuvunja mtandao wa watu wanaosafirisha kahawa nje ya nchi na kuikosesha serikali mapato.

Taarifa hiyo ya Serikali imetolewa hivi karibuni wakati Dk Tizeba alipokutana na Waziri wa Umma wa Vyama vya ushirika wa Uganda, Frederick Gume ili kutafuta suluhisho la biashara haramu ya kahawa inayofanyika mipakani.

Kulingana na TCB biashara ya kahawa hufanyika kwa njia tatu; soko la ndani ambapo wakulima huuza kwa kampuni binafsi, vikundi na  vyama vya ushirika. Pili ni kwenye mnada ambapo wasafirishaji wenye leseni hununua kahawa kutoka kwa wakulima na vyama vya wakulima; na tatu ni usafirishaji wa moja kwa moja nje ya nchi na hufanyika zaidi na wakulima wenye kahawa yenye viwango vya juu walio na mafungamano na wafanyabiashara wa kimataifa.

Kauli ya Dk Tizeba ilikuwa ni kuongeza msisitizo wa awali wa Serikali kutafuta suluhu ya bei ya kawaha ambapo wakulima wamekuwa wakilalamika kulanguliwa na madalali ambao hununua kwa bei ndogo kinyume na bei elekezi ya soko.

Mwanzoni mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF) ambao umekuwa ukilalamikiwa kuwakata fedha wakulima wa kahawa na kuagiza shughuli zote za ununuzi wa kahawa ziratibiwe na TCB.

“Kahawa itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali kwa wanunuzi wa kahawa kwenda vijijini marufuku kuanzia sasa, kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi,” alinukuliwa Waziri Mkuu.

Inaelezwa kuwa wakulima wa kahawa hasa wa mkoani Kagera, Arusha na Kilimanjaro wamekuwa wakivusha na kuingiza kahawa katika nchi za Kenya, Burundi na Uganda ambako inasemekana kuna bei nzuri ya zao hilo la biashara nchini. 

Pia wanakwepa ulanguzi wa wafanyabiashara wa ndani, bei ndogo na ucheleweshaji wa malipo yao baada ya kuuza kahawa kwenye vyama vya ushirika.  

Kwa wastani kilogramu moja ya kahawa ya Tanzania huuzwa Sh 2,000 za Uganda sawa na Dola za Marekani 0.6 huku bei ya ndani ikiwa ni Tsh. 1,460 ($0.5).


Kuhabarika zaidi:


Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa kahawa Afrika baada ya Ethiopia, Ivory Coast na Uganda ambapo kila mwaka huzalisha wastani wa tani 46,000 hadi 60,000 huku mkoa wa Kagera ukizalisha takribani tani 12,131 na theluthi moja ya kahawa hiyo huuzwa kimagendo Uganda kutokana na bei zisizotabilika nchini.

Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kahawa wa 2011/2021 unaotekelezwa na wadau wa zao hilo  unalenga kuwasajili wakulima wa kahawa nchi nzima na kuhimiza Halmashauri kutumia sehemu ya mapato yake ya kahawa kuendeleza zao na kuhakikisha mawakala wanaopunja bei ya mkulima wanadhibitiwa kwa kutangaza bei elekezi katika maeneo ya uzalishaji.

Kahawa ni zao la biashara ambalo likiwekewa mikakati linaweza kuinua maisha ya wakulima. Picha| freezone.go.ug

Wadau wataka maboresho ya bei

Wadau wa kahawa nchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya utaratibu huo wa kuuza kahawa kwenye mnada ambapo baadhi yao wanafikiri kuwa hautasaidia kutatua changamoto ya bei kwa wakulima wa kahawa. 

Mwandishi na Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Padri Privatus Karugendo katika safu yake ya gazeti moja la hapa nchini amebainisha kuwa licha ya serikali kuzuia kahawa kuuzwa kimagendo nje ya mipaka ya nchi, inapaswa kutafuta suluhu ya bei ya zao hilo ili wakulima wafaidike na soko.

“Kitendawili ambacho ambacho hakijatenguliwa hadi sasa je, kama soko la dunia la kuuza kahawa ni moja, kwa nini bei ya Burundi, Rwanda, na Uganda iwe juu na Tanzania iwe chini? Labda kutegua kitendawili hiki ni njia mojawapo ya kukomesha biashara ya magendo ili zao la kahawa lichangie kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amenukuliwaPadri Karugendo.

Hata hivyo, wengine wanafikiri kuwa utaratibu huo ni njia mojawapo ya kusaidia kuboresha maslahi ya wakulima na Serikali ipewe nafasi kutekeleza mpango huo kabla ya kuukataa.

Mwenyekiti wa Chama cha Kahawa Tanzania (TCA), John Kanjagaile amesema wadau wote washirikiane na Serikali, “Huo ni utaratibu umeshaanza kutekelezwa kuhusiana na kahawa, sina huo uwezo wa kuanza kufafanua sasa hivi, kwa hiyo tufanye kazi.”

Kanjagaile ambaye pia ni Mtendaji katika Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KCU) anabainisha kuwa hawana namna zaidi ya kutekeleza utaratibu huo kuendeleza sekta ya kahawa nchini.

Enable Notifications OK No thanks