Kigogo mwingine wa Benki ya Dunia kutembelea Tanzania wiki ijayo
Tanzania inategemea kupokea ugeni wa ngazi ya juu kutoka Benki ya Dunia ambapo Mkurugenzi wa Sera za Maendeleo na Ubia wa benki hiyo Mari Pangestu atakuwepo nchini kwa siku mbili kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan. Picha| Skills Future.
- Ni Mkurugenzi wa Sera za Maendeleo na Ubia wa benki hiyo Mari Pangestu.
- Anakua kigogo wa pili kuja Tanzania ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
- Anatakutana na Rais Samia na na wadau wa maendeleo.
Dar es Salaam. Tanzania inategemea kupokea ugeni wa ngazi ya juu kutoka Benki ya Dunia ambapo Mkurugenzi wa Sera za Maendeleo na Ubia wa benki hiyo Mari Pangestu atakuwepo nchini kwa siku mbili kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Benki ya Dunia katika taarifa yake iliyolewa leo Novemba 12, 2021 imeeleza kuwa kigogo huyo atakuwepo nchini kwa siku mbili (Novemba 15-16) ambapo moja ya shughuli yake kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia.
Pia Pangestu aliyewahi kuwa Waziri wa Utalii na Uchumi wa Indonesia kutoka 2011 hadi 2014 atapata fursa ya kuzungumza na na viongozi wengine wa Serikali pamoja na washirika wa maendeleo, wawakilishi wa vijana, wanazuoni na wasomi.
Pangestu ambaye amebobea katika kazi za utafiti na data za makundi katika Benki ya Dunia, ziara yake itajikita zaidi kujadili namna data/takwimu zinavyoweza kutumika katika kufanya maamuzi, uwazi na uwajibikaji katika shughuli za maendeleo.
Mwanamama huyo ambaye ni raia wa Indonesia pia atatembelea miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kujionea inavyotekelezwa moja kwa moja kutoka kwa walengwa.
Miradi atakayotembelea ni pamoja na mradi wa maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP), mradi wa uboreshaji mahakama na utoaji haki, mradi wa msaada wa maendeleo na takwimu Tanzania.
Soma zaidi:
Benki ya Dunia kwa sasa inafadhiri miradi 21 nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.8 (takriban Sh11.1 trilioni) hasa katika sekta za usafiri, maendeleo ya miji, elimu, nishati, maji, ulinzi wa jamii, mazingira/maliasili, maendeleo ya kidijitali na utawala.
Pangestu anakuwa kiongozi wa pili wa ngazi ya juu wa Benki ya Dunia kutembelea Tanzania katika robo ya nne ya mwaka 2021 baada Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Hafez Ghanem kudhuru nchini Septemba mwaka huu.
Ghanem alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Ziara hiyo ya Ghanem ilikuja baada ya Rais Samia kufanya mazungumzo na Rais wa benki hiyo, David Malpass kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA76) jijini New York nchini Marekani Septemba 22.
Katika mazungumzo hayo, Malpass aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa itaisaidia kukabiliana na athari za Corona (Uviko-19) na kukuza uchumi kupitia mabadiliko ya kidijitali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Aidha, Rais huyo wa Benki ya Dunia aliihimiza Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua kupitia mabadiliko sheria na sera.
Naye Rais Samia aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake kwa Tanzania katika huduma za jamii pamoja na mapambano dhidi ya Uviko-19.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Latest
