Mfahamu bosi mpya wa Benki ya Dunia Tanzania

November 10, 2022 1:18 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Nathan Belete aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Cape Verde, Gambia, Guinea-Bissau, Mauritania, na Senegal.
  • Anachukua nafasi ya Mara Warwick aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkazi katika nchi za China, Mongolia and Korea.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia imemteua Nathan Belete kuwa Mkurugenzi Mkazi mpya wa benki hiyo katika nchi za Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe akiwa ni kigogo wa tatu ndani ya taasisi hiyo Tanzania ndani ya miaka saba. 

Belete, raia wa Ethiopia na mtaalamu wa masuala ya maendeleo, anachukua nafasi ya Mara Warwick ambaye amedumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2020.

Agosti mwaka huu, Warwick alihamishwa kikazi na kwenda kuwa Mkurugenzi Mkazi katika nchi za China, Mongolia and Korea. Itakumbukwa kwa Warwick alichukua nafasi ya Bela Bird aliyeiwakilisha taasisi hiyo yenye makao yake makuu Washington, Marekani kati ya mwaka 2015 na 2020. 

Benki hiyo katika taarifa yake iliyotolewa leo Novemba 10, 2022 imesema Belete atakuwa anaendesha shughuli zake akiwa jijini Dar es Salaam ambapo atasimamia miradi ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani  bilioni 12.5 (Sh29.14 trilioni) katika nchi hizo nne zilizo chini yake. 

“Miradi hiyo ya uwekezaji inashughulikia maeneo ya kipaumbele ya mtaji wa binadamu, kilimo, miundombinu, maendeleo ya sekta binafsi, hali ya hewa, na jinsia,” imesema taarifa hiyo.

Belete mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika shughuli za maendeleo  katika bara la Afrika, Asia Mashariki, na Asia Kusini, awali alikuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Cape Verde, Gambia, Guinea-Bissau, Mauritania, na Senegal, ofisi yake ikiwa jijini Dakar.


Soma zaidi:


Kabla ya kazi za mkurugenzi mkazi, alikuwa akisimamia Idara ya Chakula na Kilimo katika kanda ya Asia Mashariki na Pacific kati ya mwaka 2014 na 2019.

“Kazi yake katika Benki ya Dunia imejumuisha kazi katika ofisi za nchi za Benki ya Dunia huko Nairobi (Kenya), New Delhi (India), na Beijing (China) na majukumu ya uwekezaji na shughuli za usaidizi wa kiufundi katika kilimo na maendeleo ya vijijini,” imeeleza taarifa ya Benki ya Dunia.

Benki ya Dunia ni mmoja ya washirika wa karibu wa maendeleo wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 50 sasa ikichagiza zaidi katika miradi ya miundombinu, biashara, na kilimo ukiwemo mradi wa awamu ya kwanza wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam wa BRT. 

Mwishoni mwa Septemba mwaka huu, benki hiyo ilitoa ufadhili  wa  Dola za Marekani milioni 335 (Sh770.5 bilioni) kwa Tanzania kwa ajili ya kupanua gridi ya Taifa ili kuwezesha upatikanaji wa umeme na usambazaji wa nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW