Rais Samia kukutana na kigogo wa Benki ya Dunia wiki ijayo
- Ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Hafez Ghanem.
- Atatembelea Tanzania Septemba 27-28, 2021.
- Atakutana pia wawakilishi wa asasi za kiraia na sekta binafsi.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Hafez Ghanem anatarajia kutembelea Tanzania wiki ijayo na atakukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.
Kigogo huyo wa Benki ya Dunia atafanya ziara ya siku mbili Septemba 27-28, 2021, kwa mujibu taarifa iliyotolewa na benki hiyo leo Septemba 24.
Mbali na kukutana na kuzungumza na Rais Samia, pia atapata fursa ya kukutana na viongozi wengine wa Serikali, wawakilishi wa asasi za kiraia na sekta binafsi.
“Ziara ya Dk Ghabem ni ya pili nchini Tanzania kama Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia,” imeeleza taarifa hiyo ya.
Ziara hiyo inakuja baada ya Rais Samia kufanya mazungumzo na Rais wa benki hiyo, David Malpass kando ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA76) unaoendelea jijini New York nchini Marekani.
Katika mazungumzo hayo, Malpass aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa itaisaidia kukabiliana na athari za Corona (Uviko-19) na kukuza uchumi kupitia mabadiliko ya kidijitali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Aidha, Rais huyo wa Benki ya Dunia aliihimiza Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua kupitia mabadiliko sheria na sera.
Naye Rais Samia aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake kwa Tanzania katika huduma za jamii pamoja na mapambano dhidi ya Uviko-19.
Benki ya Dunia imekuwa mshirika wa karibu wa Tanzania ambapo imefadhili miradi ya kitaifa 21 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.8 (Sh11.2 trilioni).
Sekta ambazo zimekuwa zikipata misaada hiyo ni pamoja na uchukuzi, maendeleo ya miji, elimu, nishati, maji, hifadhi ya jamii, mazingira, maendeleo ya kidijitali na utawala bora.
Dk Ghanem ni raia wa Misri mwenye uzoefu katika masuala ya maendeleo kwa zaidi ya miaka 30 akiisaidia Benki ya Dunia katika usimamizi wa miradi ya maendeleo hasa inayotekelezwa barani Afrika.
Kutokana na uongozi wake, Benki ya Dunia imetoa mchango mkubwa katika kutokomeza umaskini na ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea kwa kufadhili miradi ambayo inaboresha rasilimali watu, maendeleo ya sekta binafsi, ukuaji wa kilimo, mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa miundombinu bora ya kijamii na uchukuzi.
Latest
