Rais Samia awalilia masista waliofariki ajalini Mwanza
- Atoa pole kwa TEC, Jumuiya ya Masista na kwa ndugu jamaa na marafiki.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya masista wanne wa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu pamoja na dereva wao.
Rais Samia kupitia taarifa aliyoichapisha leo Septemba 16, 2025, katika ukurasa wake wa Instagram amebainisha kuwa ajali hiyo ilitokea usiku wa Septemba 15 katika kijiji cha Bukumbi Kata ya Idetemya, Tarafa ya Usagara, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.
“Ninatoa salamu za pole kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, Jumuiya ya Masista wa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, waumini wote wa Kanisa Katoliki, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda, ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wote kwa msiba huu,” imeeleza taarifa ya Rais Samia.

Mwendokasi chanzo cha ajali
Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbrod ameeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bukumbi liliokuwa likiendeshwa na Boniphace Peter Msonola (53), mkazi wa Bukumbi kuelekea jijini Mwanza kutoka Kigongo Feri.
Mtafugwa amefafanua kuwa dereva wa Land Cruiser alijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na lori aina ya Sino Truck lililokuwa likiendeshwa na Venance Manampo Mashaka (61), mkazi wa Buhongwa.
Waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na Sista Nelina Semeoni, (60), Mkuu wa Shirika la Wakarmeli wamisionari wa Mtakatifu Terezia wa Mtoto Yesu, raia wa Italia, Lilian Kapongo mkazi na Damaris Matheka.
Wengine ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana Bukumbi na raia wa Kenya Sista Stellamaris Kamene Muthin na Boniphace Peter Msonola ambaye ni dereva na mkazi wa Bukumbi wilaya ya Misungwi.
Majeruhi katika ajali hiyo ni Pauline Vicent Mipata ambaye ni msimamizi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukumbi ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya kanda Bugando.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali na hatua za kisheria zitekelezwe kwa mujibu wa sheria.
Ajali bado kitendawili Tanzania
Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani Januari-Disemba 2024 iliyochapishwa Aprili 17, 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, matukio ya ajali za barabarani yaliongezeka kwa asilimia 0.1 ambapo matukio 1,735 yaliripotiwa nchini mwaka 2024 ikilinganishwa na matukio 1,733 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Aidha, jumla ya ajali 1,170 zilizosababisha vifo ziliripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2024 zikilinganishwa na ajali 1,118 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la ajali 52 sawa na asilimia 4.7.
Latest
