Rais Samia awalilia 10 waliokufa kwa ajali Morogoro

January 2, 2026 4:30 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuzuia ajali na kulinda maisha ya wananchi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu waliopoteza maisha kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea Desemba 31, 2025 mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 2, 2026 na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano nya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu, Rais Samia ametuma salamu hizo na kuwaombea uponyaji wa haraka majeruhi wote katika ajali hiyo.

“Rais Dkt. Samia ametoa pole kwa familia za wafiwa na kuziombea roho za marehemu zipumzike kwa amani, pamoja na uponyaji wa haraka kwa majeruhi wote” imeeleza taarifa ya Kissu.

Mbali na kutoa pole, Rais Samia amewataka madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuzuia ajali na kulinda maisha ya wananchi.

Salamu za pole kutoka kwa Rais Samia zinakuja ikiwa ni siku mbili tangu kutokea kwa ajali  hiyo katika Kijiji cha Maseyu, kwenye barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam, ikihusisha basi la abiria na lori la mizigo, yaliyogongana uso kwa uso na kushika moto.

Waliopoteza maisha katika ajali hiyo kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ni wanawake wawili, wanaume nane na majeruhi 23 ambao walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu.

Kati ya majeruhi hao, 11 walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani, huku 12 wakiendelea na matibabu hospitalini.

Jeshi la Polisi limefafanua kuwa miili tisa ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, huku mwili mmoja ukiwa katika Kituo cha Afya Mikese. 

Kati ya miili hiyo, mitano imetambuliwa na familia, wakati mingine mitano bado haijatambuliwa kutokana na kuharibika kwa majeraha ya moto. Hata hivyo wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba (DNA) wamechukua sampuli kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa miili hiyo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ametoa wito kwa Wananchi wote waliopotelewa na ndugu zao kujitokeza kushiriki katika zoezi la uchukuaji wa sampuli DNA, ili kusaidia utambuzi wa miili hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks