Nane wafariki dunia kwa ajali Mwanza, 39 wakijeruhiwa
- Ni ajali kati ya basi la Asante rabi na basi la Nyehunge.
Mwanza. Watu nane wamefariki dunia na wengine 39 kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha basi la Asante Rabi iliyokuwa ikitokea Jijini Mwanza kugonga na gari la Nyehunge katika Kijiji cha Ukiriguru wilayani Misungwi.
Wilbroad Mutafungwa, Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutokea kwa ajali hiyo leo Oktoba 22, 2024, ameeleza chanzo cha ajali hiyo iliyotokea majira ya sema ajali hiyo imetokea majira ya saa 12 asubuhi .
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa kampuni la Nyehunge alipojaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake pasipo kuchukua tahadhari, eneo hili lina kona kali lakini pia kwenye eneo hili kuna alama inayomzuia kufanya hivyo na katika kukwepa sasa basi hilo likaligonga ubavu basi hilo lililokuwa linatokea Morogoro,” amesema DCP Mutafungwa.
Mutafungwa ameongeza kuwa mara baada ya ajali hiyo wananchi wamejitokeza kutoa msaada wa uokoaji wakishirikiana na watoa huduma za afya kutoka Hospitali ya Wilaya ya Misungwi waliofika katika eneo hilo.
Aidha, Mutafungwa amesema dereva wa basi la Nyehunge amejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya matibabu zaidi, huku dereva wa basi la Asante rabi akikimbia baada ya ajali hiyo kutokea.
“Jeshi la polisi linaendelea kumtafuta dereva huyo ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema Mutafungwa
Baadhi ya mashuhuda na abiria wa ajali hiyo wameambia Nukta Habari jinsi ajali hiyo kati ya magari hayo mawili ilivyotokea na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.
“Tulianza safari kutokea mkoani Morogoro majira ya saa tisa alasiri jana na tumesafiri salama. Tulipofika eneo hili tuliona gari la Asante rabi likija kwa kasi na kujaribu kuyapita magari mengine. Ghafla tukasikia mshindo mkubwa wa gari na tulipotahamaki tukaona dereva wa gari letu amebanwa na vyuma vya mlango wake na tulipogeuka nyuma tuliona gari la Asante rabi likiwa limeanguka chini,” amesema Yunis Julius abiria gari la Nyehunge.
Shuhuda mwingine Salvatory Mageni amesema aliposikia mshindo huo alidhani ni ngurumo ya radi kwa kuwa muda huo wa asubuhi mvua ilikuwa inanyesha.
“Ghafla tulisikia mtu akibisha hodi nyumbani akiomba msaada wa kumfunga kidonda chake kilichokuwa kinavuja damu na baada ya kumuuliza alieleza kuwa wamepata ajali kwenye eneo hilo la Ukiriguru,” amesema Salvatory.
Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Misungwi, Dk Clement Mwarabu amethbitisha kupokea majeruhi 39 wa ajali hiyo na kati ya hao wanne walipewa rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Amesema miili ya marehemu nane waliofariki papo kwa hapo imehifadhiwa katika kituo cha afya Iteja.
Rais Samia atuma salamu za pole
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma za pole kwa wafiwa, familia, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ajalo hiyo pamoja na ile iliyotokea mkoani Kilimanjaro.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za ajali za barabarani zilizotokea katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro na kusababisha vifo na majeruhi. Nawapa pole wafiwa wote, familia, ndugu, jamaa na marafiki. Nawaombea marehemu wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka,” amesema Rais Samia kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter.
Aidha, Rais Samia amewataka watumiaji wote wa barabara kuongeza umakini tunapoelekea mwishoni mwa mwaka,na kuzigiza mamlaka zote husika kuongeza umakini katika usimamizi wa sheria za usalama barabarani.