Rais Samia atoa pole ajali ya kuporomoka jengo Kariakoo
- Aaagiza viongozi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Jeshi la Uokozi kufanikisha zoezi la uokozi na tiba.
- Awataka Watanzania kuwaombea majeruhi na kuwatia moyo wafanyabiashara walioathirika na ajali hiyo
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Watanzania na wafanyabiashara kufuatia ajali ya kuanguka kwa ghorofa iliyotokea leo Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Kongo, Manyema na Mchikichi Dar es Salaam.
Jengo hilo linaelezwa kuporomoka majira ya saa tatu asubuhi ambapo kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.
Rais Samia aliyesafarini kuelekea nchini Brazil kuhudhuria mkutano wa G20 ametoa salamu za pole kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo amesema amesikitika kupokea taarifa ya ajali hiyo na kuwa ameshaagiza viongozi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Jeshi la Uokozi kufanikisha zoezi la uokozi na tiba.
“Nimeuagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi,” ameeleza Rais Samia.
Aidha Rais Samia amewataka Watanzania kuwaombea majeruhi kupata nafuu haraka hpamoja na kuwaombea subra ndugu jamaa, marafiki wanaotafuta riziki zao katika soko hilo la kimataifa.
kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ghorofa hilo limeanguka ghafla majira ya saa 3:05 asubuhi wakati mafundi wa ujenzi walipokuwa kazini wakitoboa kwa ajili ya kuongeza sehemu ya maduka chini ya jengo hilo.
“Tulianza kusikia kelele za mtingishiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka, wananchi wameshindwa kujiokoa na kazi ya ujenzi ilianza tangu jana, hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote,” amesema mmoja wa mashuhuda, Harrison Shayo.
Shughuli ya uokoaji inaendelea kwa wananchi wakishirikiana na vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo hadi saa 5 asubuhi bado hakuna taarifa ya moja kwa moja juu ya athari zilizosababishwa na kuporomoka kwa jengo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwa akizungumza na wananchi na wanahabari katika eneo hilo amesema majeruhi waliookolewa wamefikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hata hivyo, amesema hadi sasa idadi ya majeruhi haijafahamika wala waliopoteza maisha, akisisitiza takwimu rasmi zitatolewa baadaye.