Mfahamu Alphonce Felix Simbu Mtanzania alieshinda medali ya dhahabu mbio za marathon Tokyo

September 15, 2025 4:20 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda mbio hizo 

Dar es Salaam. Tanzania imezizima kwa furaha mara baada ya raia wake Felix Simbu kushinda medali ya dhahabu ya mashindano ya Riadha ya Dunia akimaliza katika nafasi ya kwanza upande wa mbio za Marathon Wanaume zilizofanyika usiku wa kuamkia leo huko Tokyo, Japan.

Simbu ameandika historia hiyo baada ya kumaliza mbio za kilomita 42 kwa saa 2:09.48 huku akipata upinzani mkali kutoka kwa Amanal Petros wa Ujerumani ambaye pia alikimbia muda sawa (2:09.48) na kushika nafasi ya pili, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Iliass Aouani wa Italia.

Mwanariadha huyo licha ya kumaliza muda mmoja na Petros ushindi wake umeamuliwa na teknolojia baada ya mguu wake kuwa wa kwanza kugusa ardhi baada ya kuvuka mstari wa mwisho.

Ushindi huo unamfanya Simbu kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama Mtanzania wa kwanza kushinda taji la Dunia katika riadha.

Simbu akiwa katika mashindano ya mbio za marathon Tokyo. Picha/La Voz de Galicia

Kwa kupata ushindi huo, Simbu ana uhakika wa kupata kitita cha Dola 70,000 za Marekani sawa na (Sh172 milioni) kutoka Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).

Ukiondoa Simbu, Tanzania katika mbio hizo iliwakilishwa na Josephat Gisemo aliyeshika nafasi ya 53.

Awali, Tanzania ilitarajia kupeperusha bendera yake kwa wanariadha wanne, lakini mipango hiyo ikayumba baada ya bingwa wa marathoni wa Wanawake, Magdalena Shauri na Failuna Abdi Matanga, kushindwa kushiriki kutokana na kuchelewa kupima vipimo vya jinsia vinavyohitajika na Shirikisho la Riadha la Dunia (WA).

Simbu amerudi Tokyo akiwa na kumbukumbu ya kumaliza nafasi ya saba kwenye Olimpiki 2020 kwa muda wa saa 2:11:35, lakini zaidi akiwa na historia ya kutwaa medali ya shaba kwenye mashindano ya Dunia ya mwaka 2017 London Uingereza akitumia saa 2:09:51.

Nyota huyo kutoka timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), pia ana rekodi ya saa 2:04:38 kutoka Valencia marathon mwaka jana pia nafasi ya pili Boston marathon kwa saa  2:05:04 Aprili mwaka huu.

Mtanzania wa kwanza kujinyakulia medali ya dhahabu toka mashindano hayo kuanzishwa. Picha/ The Hindu.

Pongezi kutoka kwa watu mashuhuri na viongozi zimeendelea kumiminika kwa Simbu akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na kupongeza amemtaka aendelee kujituma zaidi.

“Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa Mbio Ndefu za Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo. Ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya Taifa letu.

“Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi.

“Umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako, na hata kwa wasiyo wanamichezo,” amesema Rais Samia.

Simbu ni nani?

Ni mwanariadha aliyezaliwa Februari 14,1992 mkoani Singida, ni mume wa  Rehema Daudi na baba wa watoto.

Kwa mujibu wa tovuti ya World athletic, safari ya kimataifa ya Simbu ilianza mwaka 2011 aliposhiriki mashindano makubwa, kwa kukimbia mita 5,000 jijini Dar es Salaam na baadaye mita 10,000 kwenye michezo ya All Africa mjini Maputo.

Mwaka 2015, alishiriki kwa mara ya kwanza katika Mashindano ya Dunia ya Riadha mjini Beijing, China, kwenye mbio za marathon jambo lililompa uzoefu mkubwa wa ulingo wa kimataifa.

Mwaka uliofuata, akapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, akimaliza katika nafasi ya 5 kwa muda wa saa 2:11:15. 

Mshindi wa medali ya dhahabu Alphonce Felix Simbu wa Tanzania baada ya fainali ya mbio za marathoni za wanaume katika Mashindano ya Dunia ya Riadha 2025 yaliyofanyika Tokyo. Picha/ Xinhua/Jiang Han.

Umahiri wake ulimfanya pia ateuliwe kuwa mshikaji bendera wa Tanzania kwenye sherehe ya kufunga michezo hiyo.

Januari 2017, akawa gumzo duniani baada ya kumaliza London Marathon kwa muda wa saa 2:09:10, kabla ya kutwaa medali ya shaba ya Dunia kwenye mashindano ya riadha jijini London kwa muda wa saa 2:09:51.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW