Rais Samia atoa maagizo mazito kwa wanahabari Tanzania

May 3, 2022 1:58 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka kujilinda maana sheria na kanuni zipo bado.
  • Ataka waandike mazuri ya Tanzania na Afrika kuliko mabaya.
  • Kuimarisha zaidi uhuru wa habari.

Arusha. Rais Samia amewataka waandishi wa habari nchini kuwa waangalifu na kupima kila kitu wanachokifanya huku akisisitiza kuwa walinzi wazuri wa maisha yao na kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. 

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Mei 3, 2022 alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika jijini Arusha ambapo amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuzingatia mipaka ya kazi zao na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Amesema kwa kufanya hivyo, watajiweka katika nafasi nzuri ya kuepuka migogoro isiyokuwa na tija na mamlaka.

“Kwenu waandishi, hakuna mlinzi mzuri wa maisha yako kama wewe mwenyewe, inawezekana mtu akakwambia andika hili nitakulipa lakini unatakiwa uangalie unayoyafanya na ujipime mwenyewe kwamba nikifika hapa inatosha,” amesema Rais.

Sambamba na hilo, amewataka kuisemea vizuri Tanzania kwa sababu imepiga hatua kubwa ya maendeleo na hivyo siyo vema kwa waandishi kuandika mambo hasi tu.

“Ndani ya Tanzania tuna utajiri wa kila aina lakini waandishi wa habari wetu wengi hawaandiki hayo na badala yake mnaenda kuongea vibaya, naomba mjivunie na mkuze kilicho chenu kwani mnalindwa na Serikali, sheria za nchi na sheria za kimataifa,” amesema Rais na kuongeza kuwa,

“Waandishi wa Habari mkikaa kimya hakuna atakayelisemea bara hili hivyo wakati wengine wakizungumzia migogoro nyie zungumzieni amani na wakizungumzia umasikini zungumzieni maendeleo pia waelimisheni wananchi juu ya kuacha mila potofu.”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia Wadau mbalimbali wa Sekta ya Habari katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliofanyika Jijini Arusha tarehe 03 Mei, 2022. Picha| Ikulu.

Kuhusu kuandika habari kwa kutunza na kuheshimu mila na desturi za kiafrika, amesema uhuru wa habari hauchagui mipaka hivyo pamoja na hilo waandishi wa habari wanatakiwa kuzingatia mila na desturi za kiafrika kuandika mazuri ikiwemo vivutio vyote vilivyomo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Vyombo vya Habari na Changamoto za Kidijitali”


Elimisheni jamii kuhusu mitandao ya kijamii

Waandishi wa habari Tanzania wametakiwa kutumia nafasi zao kuchapisha maudhui yenye tija na yenye kuelimisha na kuisaidia jamii kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuwaepusha na athari hasi za teknolojia.

“Utakuta mtu anapost picha za utupu mitandaoni, mwingine anapiga picha za ajali anapost mitandaoni. Sisi serikali tataunda sheria lakini wa kwenda kuwaelimisha ni nyinyi waandishi wa habari. Wengine wanafanya kwa kutokujua na wengine wameambiwa watalipwa”, Rais Samia ameeleza katika maadhimisho hayo.

Amesema tatuwezi kukataa kuwa mitandao ya kijamii imekuwa na umuhimu katika maisha yetu, inatoa fursa ya kutumia uhuru  wa kujieleza jinsi tunavyoweza na ajira hasa kwa vijana lakini inatakiwa itumike vizuri.

Katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, Serikali imesema itaendelea kuboresha sheria zinazosimamia tasnia hiyo kwa msingi wa majadiliano na wadau mbalimbali.


Zinazohusiana:


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema sheria nyingi katika tasnia ya habari zilizokuwa zikilalamikiwa zimefanyiwa kazi hali iliyowezesha  tasnia kuwa bora.

“Tunaishukuru Serikali mpaka Septemba 2022, sheria (katika tasnia ya habari) zilizokuwa zinalalamikiwa, zitakuwa zimefanyiwa kazi,” amesema Balile.

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Afrika yamefikia kilele jijini Arusha leo ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya habari wameshiriki katika kutatafakari changamoto mbalimbali zinazokabili waandishi ikiwemo mtandaoni.

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa ni miongoni mwa waandaji wa maadhimisho hayo wakiongozwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Wadau wengine ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Twaweza, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na JamiiForums.


Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
16 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
16 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV