Tanzania yasema ‘inaheshimu uhuru wa habari’

May 3, 2021 3:46 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wadau wa habari wasema uhuru wa habari Tanzania umeporomoka.
  • Serikali yaeleza kuwa “imevipa uhuru vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema Serikali ya Tanzania inafanya kila jitihada za kuhakikisha Watanzania wanapata habari za kweli nchini kote na kwamba hadi sasa “imevipa uhuru vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”

Bashungwa amewaambia wadau wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Jijini Arusha Mei 3, 2021 kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofuata misingi, sheria na kanuni za uendeshaji wa vyombo vya habari.

“Ndugu zangu wanahabari, nyinyi nyote ni mashahidi kuwa uhuru wa vyombo vya habari hapa Tanzania ni mkubwa ukilinganisha na nchi zingine, tumesajili vyombo vingi vya habari, lakini uhuru huo uendane na wajibu, naomba sana tuhabarishe kwa kufuata misingi ya sheria, ni muhimu kufuata sheria zilizopo ili kuepukana na baadhi ya  changamoto” , Bashungwa ameeleza katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo.

Kwa takriban miaka sita sasa wadau wa habari wamekuwa wakikosoa vikali Serikali wakieleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari umeporomoka nchini jambo ambalo limepunguza ufanisi wa vyombo vya habari katika kuihudumia ipasavyo, madai ambayo Serikali inayapinga.

Awali Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile kwa niaba ya vyama vyote vya tasnia ya Habari, alisema kuna anguko la tasnia ya habari nchini Tanzania kutokana na kuzorota kwa uhuru wa habari. 

Hata hivyo, Bashungwa alipingana na hoja hiyo akieleza kuwa  kutokana na Tanzania kuwa  na uhuru wa vyombo vya habari, imefanikiwa kusajili vyombo vingi vya habari kuliko nchi yeyote Afrika kama vile Magezeti 246, Redio 194, Television 53, Redio za mtandaoni 23, blogs 120 na televisheni za mtandaoni 440.

“Nina hakika takwimu sahihi hazifiki kunakohusika, Tanzania tunaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” amesema Bashungwa.

Wadau wamekuwa wakikosoa kuwa ongezeko la vyombo vya habari nchini siyo kigezo pekee kinachoweza kuthibitisha kuwa Tanzania kuna uhuru wa habari.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa wakati akizungumza jijini Arusha Mei 3, 2021. Picha|Maelezo. 

Bashungwa, aliyekuwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo, amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinawajibika kwa kufuata sheria na kanuni za nchi ili vifanye kazi zao kwa ufanisi mkubwa katika kuuhabarisha umma wa Watanzania kwa kutenda haki na bila upendeleo wowote.

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ulimwenguni yamefikia kilele jijini Arusha leo ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya habari wameshiriki katika kutatafakari na kutafuta suluhu ya matatizo yanayovikabili vyombo vya habari yakiwemo masuala ya kiuchumi.

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa ni miongoni mwa waandaji wa maadhimisho wakiongozwa na Wizara ya habari, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) na wadau wengine kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Twaweza, LSF, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) na JamiiForums.

Maadhimisho hayo yalianza juma lililopita kwa kufanya mikutano mbalimbali ya mtandaoni na ukumbini jijini Dar es Salaam iliyohusisha mijadala na utoaji tuzo kwa wanahabari nguli wanawake waliotoa mchango mkubwa Tanzania.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW