LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni

September 30, 2019 1:07 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ile kufungiwa miezi sita kwa Kwanza Tv na faini ya Sh5 milioni kwa Ayo Tv na Watetezi Tv.
  • Imesema njia ya majadiliano na onyo ilikuwa nzuri zaidi kuliko adhabu iliyotolewa. 
  • Yashauri vituo hivyo vielemishe kuhusu sheria za utangazaji.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeishauri Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kutumia njia ya majadiliano na onyo kabla ya maamuzi ya kusimamisha au kupiga faini chombo cha habari ili kuondoa mkanganyiko wa maamuzi yanayotolewa. 

Ushauri huo umetolewa ikiwa zimepita siku mbili tangu kamati hiyo kuifungia televisheni ya mtandaoni ya ‘’Kwanza Tv’’ pamoja na kutoza faini ya Sh5 milioni kwa televisheni za  Watetezi Tv na Ayo Tv. 

Kwanza Tv ilifungiwa baada ya kukutwa na hatia ya kutoa taarifa inayohusu Dk Gwajima kupata ajali bila kutaja jina la kwanza jambo lililoelezwa kufanywa kwa makusudi kuikuza habari.

Pia Watetezi Tv na Ayo Tv zilipigwa faini hiyo kwa makosa ya kutochapisha sera na mwongozo wa watumiaji katika chaneli yake za YouTube. 

Taarifa iliyotolewa leo (Septemba 30, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga inaeleza kuwa kituo hicho kimepokea taarifa za adhabu hizo kwa masikitiko makubwa kwani inaathiri haki ya wananchi  kupata taarifa.

“Ni maoni yetu kwamba, adhabu ya kuifungia Kwanza Tv kwa kipindi cha miezi sita ni adhabu inayoathiri haki ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kupata taarifa kwa kipindi hicho kama ilivyoainishwa katika ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

“Pia, kupiga faini ya Sh5 milioni (5) Kituo cha Watetezi Tv na Ayo Tv kwa kosa la kutochapisha Sera au Mwongozo kwa Watumiaji kama inavyoainishwa na Kanuni ya 5(1) (c) ya Kanuni ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018 ni adhabu ya juu na kubwa kwa vyombo hivyo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.


Zinazohusiana:


LHRC imeeleza kuwa Kamati ya Maudhui  bila kuathiri kazi zake iwe chombo kinachosaidia vyombo vya habari kutekeleza sheria na siyo chombo cha kutoa adhabu pekee. 

“Kamati ya Maudhui itumie njia ya majadiliano na onyo kabla ya maamuzi ya kusimamisha au kupiga faini chombo. Hii ina maana ya kwamba, Kamati itoe onyo kwa maandishi endapo itabaini ukiukwaji wa sheria inazozisimamia,” anasema Henga katika taarifa hiyo. 

Septemba 3 mwaka huu, ilizitaka televisheni mbili za mtandaoni za Lemutuz Online Tv na Global Tv viombe radhi kwa siku saba mfululizo kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) ikiwemo kuonyesha na kuchapisha picha mbalimbali za ajali ya gari la mafuta iliyotokea Msamvu, Morogoro.

Enable Notifications OK No thanks