Rais Samia awashangaa wanaosema hatogombea 2025
- Ahoji nani kawaambia hatogombea.
- Awataka wanawake kushikamana kuchagua rais 2025.
- Asema ataendelea kuchagua wanawake wengi nafasi za uongozi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewashangaa watu wanaosema kuwa hatagombea nafasi ya urais mwaka 2025 huku akiwataka wanawake kushikamana ili kuhakikisha wanapata nafasi zaidi za uongozi nchini.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Septemba 15, 2021 katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam amesema wanawake wakifanya vizuri na kushikamana wanaweza kusimamisha raia mwanamke.
““Sasa ndugu zangu rais mwanamke tutamuweka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri tukishikamana tukimweka rais wetu tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana, wameaanza kutuchokoza, kuandika kwenye vigazeti Samia hatasimama nani kawaambia,” amesema Rais katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na wanawake wa Tanzania.
Amesema kuna baadhi ya watu wameanza kutumia vyombo vya habari kuvumisha uvumi kuwa hatagombea urais mwaka 2025, jambo ambalo siyo la kweli.
“Wameanza kutuchokoza kuandika kwenye vigazeti kwamba Samia hatasimama nani kawaambia?,” amehoji Rais Samia ambaye aliingia madaraka Machi mwaka huu baada ya kifo cha Rais John Magufuli.
Agosti 11, 2021 gazeti la Uhuru lilitoa habari kuwa Rais Samia hana mpango wa kugombea nafasi ya urais mwaka 2025, jambo lililozua mjadala mpana kwenye jamii na mitandao ya jamii kuhusu siasa za Tanzania miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, gazeti hilo lilifungiwa kwa siku saba kwa kile kilichodaiwa kuwa lilipotosha habari hiyo kwa sababu Rais hakuwahi kutamka kuwa hatagombea nafasi ya urais.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema wanawake wanatakiwa kutumia vizuri fursa waliyonayo sasa hasa ya kuwa na Rais mwanamke kwa sababu ni baraka kutoka kwa Mungu ya kuwainua.
“Fadhila za Mungu zikija mikononi mwaka usiziachie, wanawake wamefanya kazi kubwa kuleta uhuru katika nchi hizi, wanawake tumefanya kazi kubwa kujenga siasa za nchi hizi, tumebeba sana wanaume katika siasa za nchi hizi, leo Mungu ametupa baraka mikononi tukiachia Mungu atatulaani,” amesisitiza Rais.
Aidha, Rais Samia amesema katika uongozi wake ataendelea kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake kwa sababu wana uwezo na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
“Mtaendelea kusikia wanawake zaidi wanaingia kwenye serikali kwa sababu ninajua nisipofanya mimi, hakuna atakakuja kufanya… Tukianza hapa, atakayekuja kuvuruga huo mfumo, tutamsuta, kwa hiyo bora tuanze halafu waje waguse watuone sisi ni kina nani,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya kupata wanawake viongozi wenye sifa na vigezo stahiki, jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi.
“Ni kweli ninapopanga hizi nafasi napata shida sana kupata wanawake, siyo kwamba hawapo wapo lakini nikienda kwenye sifa na vigezo wengi wanadondoka. Nikipata kanzidata nitakuwa na wengi kuwapeleka kwenye sifa na vigezo,” amesema.
Latest
