Rais Samia akemea uvuvi haramu Mwanza, aagiza wizara kusambaza nyavu za kisasa kwa wavuvi
- Asema kuchoma nyavu na zana za uvuvi zisizofaa hakutoshi kumaliza tatizo hilo.
- Awataka wanufaika kufanyakazi kwa bidii.
Mwanza.Rais wa Samia suluhu Hassan amekemea vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika ziwa viktoria na kuagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kasi ya kusambaza nyavu ili kupambana na na vitendo hivyo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa vizimba vya ufugaji wa samaki na ugawaji wa boti za kisasa kwa wavuvi kanda ya Ziwa, leo Januari 30, 2024 amesema kuchoma nyavu na zana za uvuvi zisizofaa hakutoshi kumaliza tatizo hilo hivyo Wizara iendelee kutoa nyavu zinazotakiwa hata kwa mkopo.
“Uchomaji wa nyavu na zana za uvuvi kwa lengo la kukabiliana na uvuvi haramu kunarudisha nyuma maendeleo ya uvuvi pia kunajenga chuki kati ya wavuvi na Serikali…
…Tunachokifanya sasa utoaji wa vifaa hivi vya kisasa nina hakika nyavu zilizotolewa leo sio haramu bali ni njema hivyo nitoe rai vyema kwa wizara iendele kutoa nyavu hizo hata kwa njia ya mkopo ili wavuvi waendelee kuchukua nyavu hizo,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:Unavyoweza kuepuka ugonjwa wa ‘red eyes’
Katika hafla hiyo rais Samia amezindua ugawaji wa Vizimba vya Kufugia Samaki 222 kwa wanufaika 1,213 na Boti za Kisasa 55 kwa Wavuvi wa Kanda ya ziwa 989 zenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2.6
Uwekezaji huo ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuchochea ukuaji wa sekta ya uvuvi kupitia mpango na programu mbalimbali ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.
Mathalani, ununuzi wa meli ya kisasa ya uvuvi katika bahari kuu na ujenzi wa bandari za uvuvi katika maeneo ya Kilwa Masoko mkoani Lindi na Bagamoyo.
Huenda uwekezaji huo ukaongeza ushiriki wa wananchi wa kanda ya ziwa na maeneo jirani katika shughuli ya uvuvi.
Rais Samia Suluhu Hassan akielekeza jambo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega(kushoto) wakati akielezea kuhusu Samaki wa aina mbalimbali wanaopatikana katika Ziwa Victoria.Picha|Ikulu.
Ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/ 2020 inaonyesha kuwa kaya zinazojishughulisha na shughuli hizo nchini Tanzania ni chini ya asilimia moja.
Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya zaidi ya milioni 12 zilizopo Tanzania ni kaya 120,078 au pungufu zaidi ya hizo zinayojishugulisha na uvuvi.
Mbali na uwekezaji huo kuongeza ushiriki pia, unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa samaki amapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inabainisha kuwa ni mdogo hususani samaki wanaofugwa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa rai kwa wanufaika wa mradi huo kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuvutia wawekezaji hususani kutoka sekta binafsi.
Latest