Ulega: asilimia 10 ya fedha za halmashauri ziwanufaishe vijana

May 2, 2024 4:44 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo zitasaidia vijana kufanya uzalishaji utakaowawezesha kujikimu.
  • Waziri Ulega awataka viongozi wa usalama kufanya doria za mara kwa mara kwenye vizimba hivyo vya ufugaji.

Mwanza. Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kuvisaidia vikundi vya wajasiriamali hususani vijana ili waweze kuanzisha miradi itakayowasaidia  kujikwamua kiuchumi.

Waziri Ulega ametoa agizo hilo jana (Aprili 30,2024) wakati alipotembelea moja ya mradi wa ufugaji wa samaki wa vizimba unaofanywa na vijana wa jiji la Mwanza.

Vizimba hivyo ni miongoni vizimba 22 vilivyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 30, mwaka huu.

Katika maelekezo yake, Waziri Ulega amesema ni vizuri halmashauri zikaunga mkono jitihada zinazofanywa na vijana hao katika kuwapatia mkopo wa asilimia 10 unaotarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni ili waweze kufanya uzalishaji utakaowawezesha kujikimu.

“Tunakaribia kufungua dirisha la kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wajasiriamali, niombe fedha hizi zitolewe kwa wingi kwa makundi haya ili waweze kufanya uzalishaji wa kujiongezea kipato,” amesema Waziri Ulega

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewataka viongozi wa usalama kuhakikisha wanafanya doria za mara kwa mara kwenye vizimba hivyo vya ufugaji ili kukamata waharamia wanaoweza kuharibu vizimba hivyo na kuiba samaki.


Soma zaidi:Rais Samia akemea uvuvi haramu Mwanza, aagiza wizara kusambaza nyavu za kisasa kwa wavuvi


“Kwa yeyote atakayejaribu kufanya uharibifu wa vizimba hivi achukuliwe hatua za kisheria,”amesema Ulega

Akizungumzia maelekezo hayo, Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema tayari ofisi yake imetenga zaidi ya Sh100 bilioni zitakazotolewa kwa wajasiriamali hao.

“Tumepokea maelekezo yao na sisi kama halmashauri tumetenga kiasi cha Sh100 bilioni na zinasubiri kuidhinishwa ili zianze kutumika na kwenye mradi huu tutaleta zaidi ya Sh400 hadi 500 milioni ili ziweze kusaidia ufugaji,” amesema  Kibamba

Awali akizungumzia kuhusu mradi wa ufugaji wa samaki katika vizimba vilivyopo mtaa wa Kisoko jijini Mwanza, Katibu wa wanufanika wa vizimba hivyo, Pius Mtenya amesema mradi una vizimba 60 na una jumla ya vifaranga milioni 4.5.

Pamoja na mafanikio hayo, wajasiriamali hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, ukosefu wa taa za umeme jua zinazoweza kutazama mradi wote, boti 40 kwa ajili ya doria ya usiku, changamoto ya magugu maji na uhaba wa vibanda vya ulinzi na wavuvi kusogea kwenye mradi kutokana na ukosefu wa mpaka (bikoni). 

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Nukta TV

Tunachokifahamu kuhusu ziara ya Rais Samia Urusi, kidiplomasia na uchumi

Tunachokifahamu kuhusu ziara ya Rais Samia Urusi, kidiplomasia na uchumi

Nukta TV

Kutoka Ubunge hadi mshauri wa Rais, Panda shuka ya Ummy Mwalimu katika siasa

Kutoka Ubunge hadi mshauri wa Rais, Panda shuka ya Ummy Mwalimu katika siasa

Nukta TV