Mawaziri waliotemwa na Rais Samia wateuliwa kamati za Bunge
- Ni Dk Kalemani, Dk Ndungulile na Mhandisi Dk Chamriho.
- Wametuliwa katika Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
- Rais Samia aliwatengua.
Dar es Salaam. Mawaziri watatu akiwemo aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ambao nyadhifa zao zilenguliwa hivi karibuni wamepata teuzi katika kamati za kudumu za Bunge la Tanzania.
Uteuzi huo umekuja baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kufanya mabadiliko madogo ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 135 (3) – (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020.
Aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
Dk Kalemani ambaye ni Mbunge wa Chato na aliyekuwa Waziri Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dk Leonard Chamuriho wameteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo.
Rais Samia alitengua teuzi za mawaziri hao watatu Septemba 12, 2021 kwa kile kilichodaiwa kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.
“Katika kipindi cha miezi sita kuna watu waliichukulia hiii serikali poa, serikali cool, watu wakafanya wanayoyataka… kutokana na jinsi nilivyoona utendaji wa mawaziri na viongozi wengine kwenye wizara, mabadiliko haya bado yatakuwa yanaendelea,” alisema Rais Samia Septemba 13 wakati akiwaapisha mawaziri wapya aliowateua.
Pia Spika Ndugai amemuhamisha Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi kutoka Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Humphrey Polepole ambye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa amehamishiwa kwenda Kamati ya Sheria Ndogo.
Wabunge wa Viti Maalum, Asia Halamga na Agnes Marwa wameteuliwa kuwa mjumbe ya Kamati ya Masuala ya Ukimwi.
Latest