Majanga: Asilimia 80 ya kidato cha nne wafeli hesabu Tanzania

January 31, 2023 11:53 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu hafifu katika mtihani huo wa kidato cha nne unafanya hesabu kuwa somo ambalo ufaulu wake ni ‘tiatia maji’. 
  • Masomo ya sayansi nayo yanahitaji mbinu mpya, mambo bado magumu.
  • Watahiniwa takriban wanne kati ya 10 waangukia pua somo la Historia.

Dar es Salaam. Licha ya kuongezeka kwa shinikizo la kuongeza ubora wa ufaulu katika masomo ya hesabu na sayansi nchini Tanzania miaka ya hivi karibuni, hali bado mbaya baada ya asilimia 80 ya watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne kufeli somo la hisabati. 

Katika matokeo ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2022, yaliyotangazwa leo Januari 29, 2023 na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Athuman Amas ni asilimia 21.1 tu ya wanafunzi ndiyo wamefaulu somo hilo muhimu katika kumwandaa mwanafunzi kuwa na fikra tunduizi. 

Hii ina maana kuwa ni watahiniwa wawili tu kati ya 10 waliofanya mtihani wa hisabati Novemba 2022 ndiyo wamefaulu. 

Hesabu ni moja ya masomo muhimu katika ukuzaji wa sayansi na teknolojia katika taifa lolote ulimwenguni. 

Kumekuwa na mfululizo wa matokeo mabaya katika somo la hisabati pamoja na masomo ya Sayansi katika matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi, upimaji kitaifa kidato cha pili na mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.

“Katika somo la Basic Mathematics (Hisabati), watahiniwa 415, 844 wamepata daraja F ambao ni sawa na asilimia 79.9,” Amas amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam. 

Hiyo inamaanisha kwamba wanafunzi nane kati ya 10 wamefeli somo hilo ambalo linatumika katika maisha ya kila siku.



Si Baiolojia, si Kemia hali si hali

Katika masomo ya sayansi, somo la Baiolojia limeonekana kuwaumiza vichwa zaidi watahiniwa wa kidato cha nne mwaka 2022, ambapo asilimia 32, ya watahiniwa wamefeli somo hilo wakifuatiwa na somo la Fizikia ambapo watahiniwa wamefeli kwa asilimia 31. 

Kwa matokeo hayo, kati ya watahiniwa watatu waliofanya mtihani wa Baiolojia mwaka jana, mmoja tu ndiyo ametoboa huku wengine wawili wakilala chali. 

Uchambuzi wa matokeo uliofanywa na Nukta Habari, umebaini watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika mtihani wa Kiswahili katika kundi la masomo ya lugha.

Katika masomo hayo ya lugha, asilimia nne ya watahiniwa au watahiniwa wanne kati ya 100 pekee wamefeli Kiswahili. 

Hata hivyo, ni kinyume kwenye somo la Kiingereza baada ya asilimia asilimia 31 kufeli somo hilo. Kwa lugha nyepesi, wanafunzi watatu kati ya 10 waliofanya mtihani wa Kiingereza wamefeli kabisa. 

Itakumbukwa mara baada ya matokeo ya Mtihani wa Upimaji Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) mwaka 2022, wadau mbalimbali wa elimu akiwemo Richard Mabala waliishauri Serikali kutupia macho lugha ya kufundishia kwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha wanafunzi kufeli.

Hata Historia bado mambo magumu

Mbali na Kiingereza, somo la Historia nalo limeonekana kuwa mfupa mgumu kutokana na watahiniwa 193, 483 kupata daraja F sawa na asilimia 38 ya watahiniwa wote. 

Ufaulu huo umelifanya somo la Historia kuwa miongoni mwa masomo ambayo wanafunzi wamefanya vibaya.

Pamoja na takwimu kuonesha zaidi ya nusu ya watahiniwa wamekuwa wakifaulu masomo ya sanaa na lugha bado juhudi mpya zinatakiwa ili kuongeza idadi ya wanaofaulu tofauti na sasa ambapo asilimia 30 ya watahiniwa wamefeli somo la Uraia huku asilimia 33 wakifeli somo la Jiografia.

Licha ya kutokuwepo kwa idadi kubwa ya vitabu vya masomo ya biashara katika shule za Sekondari, kiwango cha ufaulu kipo juu kiasi kulinganisha na masomo mengine.

Mathalani ni asilimia 13 tu ya watahiniwa waliofeli somo la Commerce huku wanafunzi 2,032 sawa na asilimia 16 wakifeli somo la Book-keeping.

Huenda uwiano huo unachangiwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaosoma masomo hayo ambayo sio ya lazima katika shule za Sekondari.


Tangazo:

Enable Notifications OK No thanks