Somo la kompyuta lilivyowatoa jasho watahiniwa kidato cha sita 2022
- Ni watahiniwa wawili kati ya 10 ndiyo wamefaulu.
- Kiswahili chawapunguzia maumivu, wafaulu kwa asilimia 100.
- Wadu washauri kuongeza uwekezaji somo la kompyuta.
Dar es Salaam. Kwa kawaida imezoeleka kuwa masomo ya hesabu na sayansi huwatoa jasho zaidi wanafunzi katika ngazi zote za elimu, basi leo fahamu kuwa somo la kompyuta ndiyo lilikuwa pasua kichwa kwa watahiniwa wa kidato cha sita mwaka 2022.
Uchambuzi wa takwimu za ufaulu kwa masomo za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) uliofanywa na nukta.co.tz unaonyesha kuwa ni asilimia 22.15 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu ndiyo wamefaulu somo hilo.
Hiyo ni sawa na kusema watahiniwa nane kati ya 10 wamefeli somo la kompyuta ambalo ni muhimu katika ulimwengu wa kidijitali.
Ufaulu huo mbaya ni wa kushtua kwa sababu umeporomoka kwa kasi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Mwaka jana asilimia 60.52 ya watahiniwa walifaulu somo hilo.
Masomo mengine ambayo ufaulu wake umeshuka mwaka huu ni General Studies, Geography na Basic Applied Mathematics.
Hata hivyo, ufaulu wa masomo hayo haujashuka chini ya asilimia 90 isipokuwa Basic Applied Mathematics, ambalo watahiniwa wake wamefaulu kwa asilimia 58.66 kutoka asilimia 60.85 mwaka jana.
Soma zaidi:
-
Matokeo kidato cha sita 2022 haya hapa
-
Matokeo kidato cha sita 2022 yatangazwa, ufaulu waongezeka kidogo
Wakati masomo hayo yakiwa na ufaulu wa chini kuliko mengine, watahiniwa wa mwaka huu wamefanya vizuri katika masomo ya History, English Language, French Language, Arabic Language na Physics.
Chemistry, Biology, Agriculture, Advanced Mathematics, Economics, Accountancy na Food and Human Nutrition umepanda ikilinganishwa na mwaka 2021.
“Ufaulu katika somo la Commerce ni asilimia 99.85 sawa na mwaka 2021. Ufaulu katika somo la Kiswahili ni asilimia 100 sawa na ufaulu wa somo hilo kwa mwaka 2021,” alisema Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amas alipokuwa akitangaza matokeo hayo wiki hii.
Wakati hesabu zikitajwa kuwa ugonjwa wa Taifa kwa wanafunzi wengi, huenda somo la kompyuta nalo linatakiwa kuongezwa katika orodha hiyo ili kuwapa fursa wadau wa elimu kutafuta tiba ya wagonjwa hao.

Mtaalam wa programu za kompyuta, Sogwejo Florian amesema ili mwanafunzi afaulu somo la kompyuta anatakiwa kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.
“Huenda wamefeli zaidi labda hawakuwa na vifaa vya kutosha katika shule zao,” amesema mtaalam huyo.
Amesema pia uelewa wa wanafunzi unategemea walimu wanaofundisha somo husika na ikiwa mwalimu hana maarifa ya kutosha kuhusu kompyuta hawezi kutoa maarifa na ujuzi unaotakiwa kwa anaowafundisha.
Ameshauri uwekezaji uongezwe katika masomo ya sayansi hasa kompyuta kwa sababu kazi nyingi hutegemea kifaa hicho na ili kuzalisha wahitimu bora, wadau wa elimu na Serikali wakae pamoja kutafuta ufumbuzi.
Latest